SERIKALI YAPATA MSAADA WA KUWAPATA WENGINE VIONGOZI WA SIMBA

WAKILI wa Serikali Mwandamizi, katika kesi inayowakabili viongozi wa Simba SC, Shadrack Kimaro amesema kwamba wamepata msaada wa Interpol kwa ajili ya kuwapata watuhumiwa wengine, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu, Zacharia Hans Poppe na Franklin Lauwo.
Lakini Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, Thomas Simba amesema kwamba mahakama ilikwishatoa amri kwa upande wa Jamhuri kufanya marekebisho ya hati ya mashitaka ya kuwaondoa Poppe na Lauwo ili kesi iweze kuendelea kwa watuhumiwa wengine, Rais wa Simba SC, Evans Aveva na Makamu wake, Geoffrey Nyange maarufu Kaburu.
Hakimu Simba alitoa amri hiyo baada ya mawakili wa Aveva na Kaburu kuwasilisha maombi ya kutaka kutupiliwa mbali kwa hati ya mashitaka kutokana na uwepo wake usio sahihi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe sasa anatafutwa na Interpol
Baada ya Hakimu Simba kumkumbusha suala hilo, wakili Kimaro aliomba wapangiwe tarehe ya usikilizwaji wa awali ambapo hakimu alipanga Agosti 3, mwaka huu.
Hakimu Simba ametoa uamuzi huo leo baada ya Wakili Kimaro kuiomba mahakama kupangiwa tarehe ya usikilizwaji wa awali mbele ya Aveva ambaye leo hakuwapo mahakamani hapo kutokana na kuwa mgonjwa huku Kaburu akiwapo mahakamani hapo.
Awali, Kimaro aliitaarifu mahakama kwamba shauri hilo kuanzia sasa litakuwa likiendeshwa na mawakili kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) wakishirikiana na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Pia alidai wamepata msaada wa Interpol kwa ajili ya kuwapata Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe na Franklin Lauwo.
Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashitaka ya kula njama, matumizi mabaya ya madaraka, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, utakatishaji fedha na kuandaa taarifa ya uongo.
Katika mashtaka hayo, Poppe anadaiwa kughushi, kutoa maelezo ya uongo huku Lauwo akikabiliwa na shitaka moja tu la kuendesha biashara ya ukandarasi kinyume na sheria.

LihatTutupKomentar