KAIMU Rais wa klabu ya Simba SC ya Dar es Salaam, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema kwamba kiungo Mnyarwanda Haruna Hakizimana Fadhil Nyonzima atachukuliwa hatua za kinidhamu kwa kuchelewa kurejea nchini kujiunga na timu baada ya ruhusa maalum aliyopewa.
Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini Dar es Salaam, Abdallah amesema kwamba Haruna alipewa ruhusa maalum ya hadi Julai 20 awe amerejea kuungana na wenzake kwa safari ya Uturuki, lakini ajabu hadi leo hajarudi.
Amesema kwamba tayari pasipoti yake ilikuwa imekwishagongwa visa kwa safari ya Uturuki kwenye kambi ya maandalizi ya msimu mpya pamoja na wenzake, lakini kutokana na kuchelewa ameshindwa kwenda.
Haruna Nyonzima atachukuliwa hatua za kinidhamu kwa kuchelewa kurejea Simba SC
Abdallah amesema kwamba alitarajia Niyonzima baada ya kukosa matayarisho ya mwanzoni mwa msimu uliopita, kiasi cha kusumbuliwa na maumivu baadaye yaliyomuweka nje muda mrefu, safari hii angejitahidi kuwahi kushiriki mazoezi ya awali ili awe fiti zaidi, lakini imekuwa tofauti.
“Haruna ni mchezaji wa Simba, tulimpa ruhusa maalum ya mapumziko na matibabu kule kwao, Rwanda na tarehe ambayo alitakuwa kurudi Haruna ilikuwa ni tarehe 20, ili aweze kuungana na wenzake, na hata pasipoti yake tayari ina visa ya Uturuki, lakini kwa sababu ambazo tumeshindwa kuzifahamu mpaka sasa hajajiunga na timu,”amesema Abdallah.
Ameongeza kwamba wao kama viongozi wanajaribu kuangalia sababu za Haruna kutotokea kwenye kambi ya maandalizi ya msimu mpya kwa kufuata taratibu za kunidhamu, kwanza kwa kumuhoji ajieleze juu ya kuchelewa kwake na ikionekana ana makosa ataadhibiwa.
Hata hivyo, Abdallah ameonyesha ana imani kubwa na Haruna kwamba akiwa fiti anaweza kuisaidia timu, lakini amesema kwa sasa hawezi kwenda tena kwenye kambi ya Uturuki bali akirejea anaweza kupewa programu maalum ya peke yake na mwalimu.
Wachezaji wote wa Simba SC wapo kambini katika hoteli ya Reen Park & Resorts mjini Istanbul kwa maandalizi ya msimu mpya chini ya kocha wake mpya, Mbelgiji Patrick J Aussems anayesaidiwa na Mrundi, Masoud Juma, Mtunisia Adel Zrena Kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili na Muharami Mohammed ‘Shilton’ kocha wa makipa.
Na Simba SC inatarajiwa kuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Mouloudia Club of Oujda ya Morocco Jumatano wiki ijayo Uwanja wa Kartepe Green Park mjini Istanbul kuanzia Saa 10:00 kwa saa Saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Wachezaji waliopo huko ni makipa; Aishi Manula, Deogratius Munishi ‘Dida’ na Ally Salim. Mabeki ni Shomali Kapombe, Asante Kwasi, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Nicholas Gyan, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Yussuf Mlipili, Paul Bukaba, Vincent Costa na Salim Mbonde.
Viungo ni James Kotei, Jonas Mkude, Muzamil Yaasin, Shiza Kichuya, Cletus Chama, Haruna Nionzima, Hassan Dilunga, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim, Marcel Kaheza, Abdul Hamisi, Rashid Juma na Said Ndemla.
Washambuliaji ni Emmanuel Okwi, John Bocco, Meddie Kagere, Adam Salamba na Mohammed Rashid.
Kikosi kinatarajiwa kurejea nchini Agosti 6 tayari kwa tamasha la kila mwaka la klabu, Simba Day ambalo hufanyika Agosti 8 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam