Dar es Salaam. Kucheza chini ya kiwango kwa safu ya ushambuliaji ya Yanga katika mechi saba za kimataifa, zimewaweka wawakilishi hao wa Tanzania katika nafasi finyu ya kutimiza ndoto ya kufika hatua za juu kwenye mashindano hayo.
Yanga ambayo muda mrefu imekuwa na ndoto ya kufuzu angalau hatua ya nusu fainali kwenye mashindano hayo, tayari imeshindwa kufanya hivyo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuondolewa katika raundi ya kwanza na Township Rollers ya Botswana.
Pia kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu, Yanga ina nafasi ndogo ya kuingia hatua ya robo fainali, hatua ambayo kwa kiasi kikubwa imechangiwa na ubutu wa safu ya ushambuliaji.
Dalili za majanga ya safu ya ushambuliaji ya Yanga zilianza kuonekana mapema kwenye raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kupenya kwa taabu mbele ya vibonde St. Louis ya Shelisheli kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1.
Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 nyumbani kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 ugenini, lakini washambuliaji walishindwa kuibeba kwenye raundi ya kwanza mbele ya Rollers ambapo ilifungwa nyumbani mabao 2-1 kabla ya kwenda kutoka suluhu nchini Botswana, siku kumi zilizofuata.
Baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa, Yanga ilitua mikononi mwa Welayta Dicha ya Ethiopia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ambapo safu ya ushambuliaji ilijitutumua, baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani, ingawa tatizo lilijirudia kwenye mechi ya marudiano nchini Ethiopia ambapo ilifungwa bao 1-0.
Matokeo hayo yaliivusha Yanga hatua ya makundi ambayo katika mechi tatu ilizocheza kabla ya mchezo wa nne jana, safu yake ya ushambuliaji ilishindwa kufunga hata bao moja ilipocheza na timu za USM Algers, Rayon Sports na Gor Mahia.
Yanga ilipoteza mbele ya USM Algers kwa mabao 4-0, ilitoka suluhu na Rayon Sports kabla ya kuchezea kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Gor Mahia, ugenini Kenya siku 11 zilizopita.
Kabla ya mchezo wa jana, Yanga ilikuwa imefunga mabao sita tu katika michezo tisa ya kimataifa ambayo ilikuwa imecheza mwaka huu.
Hadi wakati inaingia uwanjani kwenye mchezo wa jana, Yanga ilikuwa na deni la kusaka pointi tatu kufufua matumaini ya kufuzu hatua ya robo fainali, lakini ina deni jingine la kuhakikisha inafunga mabao mengi kupunguza utofauti isiyovutia ya mabao ya kufunga na kufunga iliyokuwa nayo kabla ya mechi ya jana.
Yanga ina mtihani mwingine wa kuibuka na ushindi kwenye mechi mbili zilizobaki dhidi ya USM Algers na Rayon Sports, pia ina kibarua kingine cha kuombea wapinzani wake wafanye vibaya kwenye mechi walizobakiza jambo ambalo linaonekana kuwa gumu.
Katika kudhihirisha washambuliaji wanavyoigharimua Yanga kwenye mashindano ya kimataifa, timu hiyo imelazimika kuongeza ‘nyota’ wawili katika nafasi tatu za usajili wa nyongeza ambazo walikuwa nazo kwenye mashindano hayo.
Washambuliaji walioongezwa na Yanga ni Heritier Makambo na Matheo Anthony lakini pia kuna jina la kiungo mshambuliaji, Mohammed Issah 'Banka'.
"Nadhani kikubwa kilichotuangusha ni majeruhi kwani tumecheza mechi nyingi tukiwa na kikosi ambacho hakijakamilika hivyo ni vigumu kupata muunganiko mzuri katika hali kama hiyo.
Lakini pia hata washambuliaji wenyewe nao hawakuwa na umakini wa kutumia nafasi ambazo tumekuwa tukizitengeneza ingawa naamini tatizo hilo linarekebishika na tutakuwa vizuri tu," alisema Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera.
Matokeo ya Yanga Kimataifa
Yanga 1-0 St Louis
St Louis 1-1 Yanga
Yanga 2-1 Township Rollers
Township 0-0 Yanga
Yanga 2-0 Welayta Dicha
Dicha 1-0 Yanga
USM Algers 4-0 Yanga
Yanga 0-0 Rayon
Gor Mahia 4-0 Yanga