JE USIKU WA LEO JINA LA ALI KIBA LITAONEKANA COSTAL UNION

LEO saa 6:00 usiku dirisha la usajili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Daraja la Kwanza na Daraja la Pili ambalo lilifunguliwa Juni 6, mwaka huu, litafungwa.

Wakati dirisha hili likitarajiwa kufungwa leo, moja ya usajili mkubwa ambao unasubiriwa kama utakamilika ni ule wa mwimbaji wa Bongo Fleva, Ali Kiba.

Kwa siku kadhaa sasa mashabiki wa soka nchini wamekuwa wakisubiria kwa hamu kusikia kukamilika kwa usajili wa msanii huyo kwenda Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’.

Lakini swali kubwa juu ya dirisha hilo la usajili lililofunguliwa Juni 15, mwaka huu na leo saa 6:00 usiku timu zote zitakuwa zimekamilisha taratibu za kuwanasa wachezaji wanaowataka, lakini ule ambao umeonekana kuteka masikio ya watu wengi wa Kiba mpaka sasa bado haujakamilika.

Wadau wengi wa soka wamekuwa wakijiuliza juu ya usajili huo kama utakuwa na msaada wowote kwa Coastal Union, huku wengine wakidhani ni sula zima la kiki.

Lakini ukweli ni kwamba, kuna mambo ambayo Kiba ataisaidia Coastal Union ikiwa watafanikisha usajili huo kabla ya dirisha hili kufungwa.

Moja ya jambo ambalo Kiba atawasaidia mabingwa hao wa Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu Tanzania Bara) mwaka 1988, Coastal Union, ni hamasa kwa mashabiki.

Kwasasa hamasa ni tatizo kubwa kwa mashabiki wa Coastal Union, kutokana na timu hiyo kushuka daraja mara kwa mara.

Ambapo mwaka 2002, Coastal Union walishuka daraja na kubakia kwenye ligi za chini kwa muda wa misimu mitano na kurejea Ligi Kuu msimu wa 2007/08 na kushuka msimu huo huo.

Msimu wa 2010/2011, Coastal Union ilipanda daraja na kucheza Ligi Kuu msimu wa 2011/2012 na kufanikiwa kumaliza nafasi ya tano, ambapo walidumu kwa misimu mingine mitatu kabla ya kushuka tena 2015/2016.

Msimu huo wa 2015/2016, ulikuwa mbaya zaidi kwa mashabiki wa Coastal Union, baada ya timu zote tatu za Tanga (Coastal Union, African Sports na Mgambo JKT) kushuka daraja.

Hivyo hali hiyo imepoteza kabisa hamasa ya mashabiki wa soka wenye mzuka mkoani Tanga, hasa kitendo cha kushushwa kwa timu zote tatu.

Hadi leo mashabiki wa soka wa Tanga hawaamini kama timu zao zilishuka kihalali, wakiamini kwamba ulikuwa mpango wa watu wasiokuwa na nia njema na mkoa huo na ndio maana mashabiki walikuwa wakionyesha hasira zao kwa kuwapiga waamuzi.

Hivyo usajili huo unaweza ukawahamasisha mashabiki waliopotea kwenye mechi za Ligi Kuu kuanza kuhudhuria tena, huku hata wale wapenzi wa muziki wasio mashabiki wa soka watakuwa wakiifuatilia timu hiyo.

Jambo la pili ambalo Kiba ataweza kuisaidia Coastal Union, ni mauzo ya jezi hizo kwa mashabiki wa soka mkoani Tanga.

Lakini pamoja na mashabiki wa Coastal Union, kuna wale wa timu nyingine wanaompenda Kiba wanaweza kununua jezi, biashara ambayo itaongeza uchumi wa timu hiyo ambao ni mbovu kama zilivyo timu nyingine za Ligi Kuu.

Pamoja na mambo hayo mawili ya nje ya uwanja ambayo Kiba ataweza kuwasaidia Coastal Union, lakini msanii huyo si wa kumbeza kwa upande wa uchezaji wake wa soka.

Kipaji cha Kiba kwenye soka ni cha kiwango cha juu, hata baadhi ya makocha kama Jamhuri Kihwelu amewahi kuzungumzia hilo baada ya mechi ya kati ya Team Kiba na Samatta iliyokuwa ya kuchangia elimu.

“Siku zote mimi nasema Ali Kiba ni mchezaji mzuri sana, tena anawazidi wachezaji wengi wa Ligi Kuu Tanzania Bara,” anasema Kihwelu.

“Kila timu niliyoenda kufundisha nilikuwa namwambia nimsajili, kama atashindwa kuja mikoani acheze hata mechi za Dar tu.”

“Mimi ni kocha mzoefu hapa nchini na ninawafahamu wachezaji wengi sana na ninasema, Kiba ni mchezaji mahiri na angeamua kucheza mpira basi angecheza mwaka mmoja tu hapa Bongo kabla ya kutimkia nje,” aliongeza Kihwelu.

Hivyo, Coastal watafaidika nje na ndani ya uwanja ikiwa leo watafanikiwa kukamilisha dili la kumsajili msanii huyo wa Bongo Fleva.

LihatTutupKomentar