GUMZO la mashabiki ni kwamba Beno Kakolanya anaweza kumuweka benchi Aishi Manula?Amesaini mkataba wa miaka miwili Msimbazi. Lakini ametamka kwamba; “Moto utawaka.”
Kakolanya kujiunga na Simba ni wazi vita ya namba itazidi kukolea kwenye kikosi hicho ambacho kinaongozwa na Tanzania One, Aishi Manula akisaidia na Deo Munishi ‘Dida’ na Ally Salum.
Kirekodi ushindani utazidi kuwa mkubwa lakini Manula bado ataendelea kuwa bora kutokana na kuwa na rekodi bora zaidi na kwenye ligi akionekana kuwa vizuri zaidi.
Lakini makipa hawa kila mmoja anarekodi yake katika msimu uliomalizika hivi karibuni wa 2018/19 ambao Simba ilikuwa bingwa.
Katika msimu uliopita, Kakolanya akiwa na Yanga alicheza mechi nane tu za Ligi Kuu Bara na kwenye michezo hiyo miwili pekee ndiyo aliruhusu mabao.
Hivyo Kakolanya alikuwa ana ‘clean sheet’ sita katika mechi nane ambazo alicheza akiruhusu bao mechi ya Mtibwa ambayo walishinda 2-1 na sare dhidi ya Ndanda 1-1.
Huku Manula yeye akionekana kuwa bora zaidi kuliko wenzake wake baada ya kucheza mechi 29 na kutoa jumla ya ‘clean sheet’ 21 kati ya mechi ambazo alidaka kwenye ligi kuu.
Huku Dida akidaka mechi tisa na katika mechi hizo mbili aliweza kuruhusu mabao mechi dhidi ya Biashara 1-1 na KMC 2-1.
Kwa upande wa Ally Salum ambaye ni kipa kinda yeye alicheza mechi moja baada ya Manula kuumia na kutolewa ukiwa ni mchezo wa pili wa ligi wa msimu uliomalizika dhidi ya Mbeya City na Simba ilishinda mabao 2-0 katika Uwanja wa Taifa.
kipa huyo mpya, Beno Kakolanya na akafunguka mwenyewe: “Suala la ushindani wa namba kati yangu na Manula na Dida siwezi kusema mimi lakini kocha ndiye atakayeamua kati yetu nani ana kiwango bora na aweze kumtumia na kumpanga uwanjani.”
“Nimejipanga vizuri kupambana na kupata namba ndani ya Simba sababu nilipokuwa nje sikuwa nimekaa tu bali nilijiandaa na kufanya mazoezi kwa bidii zote na hilo litaonekana,”alisema Kakolanya ambaye aliwahi kutamba na Prisons ya Mbeya.