RASMI mashabiki wa Yanga wasahau kuona ule udambwiudambwi wa nahodha wao, Ibrahim Ajibu. Amewaaga na anakwea pipa kwenda kuanza changamoto mpya DR Congo na timu yake ya TP Mazembe.
Spoti Xtra linajua kwamba dau la Ajibu mezani ni Milioni 120 na Yanga haitanufaika nalo kwavile alishamaliza mkataba nao.
Meneja wa mchezaji huyo, Athuman Ajibu amesema kuwa mambo ni moto mteja wake anaondoka jumla muda wowote kuelekea Congo kwani mazunguzo yamefika patamu.
“Mambo kwa sasa ni moto, Ajibu anasepa zake Yanga na kuhusu dau lake na masuala mengine muhimu tutazungumza ila kwa sasa habari ni kwamba anaondoka Yanga anakwenda Mazembe,” alisema Ajibu.
Alipotafutwa Ibrahim Ajibu azungumzie suala hilo hali alijibu kifupi tu “Ni jambo jema kwangu na timu yangu.”
AMTAJA MANARA
Ajibu ameaga mashabiki wake jana huku akimtaja Haji Manara kuwa ni mmoja ambao wamemfanya afanikiwe.
Alisema maneno hayo kupitia ukurasa wake wa Instagram ambao ulisomeka hivi; “Nimepitia katika klabu nyingi sitaacha kuwashukuru Simba maana ndiyo walionifanya kufika hapa kwa nafasi ya pekee Haji Manara amekuwa mtu wa hamasa kutoa moyo pamoja na kujenga saikolojia ya kila mchezaji anastahili heshima.
“Pongezi kwa Yanga miaka miwili imekuwa bora kwangu licha ya changamoto za kimaisha ila upendo wa mashabiki wake ni mwingi nashindwa cha kuwalipa zaidi ya asante mlitujali, heshima, utu na licha ya kuwaudhi na kuwakera ila mlisahau yote nitawakumbuka kwa mema yote, viongozi benchi la ufundi na kila mmoja kwa mchango wake zaidi Mungu awabariki.”