TUZO ZA SINEMA ZETU 2019 ZAZINDULIWA RASMI

TUZO ZA SINEMA ZETU 2019 ZAZINDULIWA RASMI


Hatimaye Kituo cha Azam TV kupitia chaneli yake ya Sinema Zetu, leo Jumanne imezindua rasmi msimu mpya wa tuzo zao za Kimataifa za Sinema Zetu, ambapo Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando, amesema taratibu zote za maandalizi kuelekea msimu huo mpya zimeshakamilika na kwamba zitaanza rasmi Januari Mosi, mwakani na kuhitimishwa Februari 23 katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia maboresho ya tamasha hilo kwa msimu wa pili, Tido alisema, kwa kuwa mwanzo wao umeonekana kupokelewa vizuri na washiriki husika, mwakani watahakikisha mshiriki yeyote anawasilisha filamu iliyoandaliwa kuanzia mwaka 2016 hadi 2018, kwani hiyo ndiyo njia pekee inayoweza kuwapa picha halisi ya ufanisi na ubora wa uandaaji wa filamu.

“Kila mtu anatakiwa kujua kuwa kwa sasa Kiswahili ni miongoni mwa lugha kumi kubwa kuzungumzwa Barani Afrika, hivyo tumeamua kufanya tamasha la tuzo hizi ili iwe njia moja ya kufikisha Lugha ya Kiswahili kwa watumiaji wapya kwani tuzo hizo zitashindanisha takribani mataifa yote ya Afrika ambayo yameshakubali kushirikiana nasi.

“Uwasilishaji wa kazi hizo utaanza mara moja Oktoba Mosi, mwaka huu mpaka Novemba 30, mwaka huu, mchakato wote huo wa upokeaji wa kazi za wasanii utakuwa chini ya COSOTA na Bodi ya Filamu Tanzania, huku mwenyekiti wa jopo la majaji atakuwa ni profesa Martin Mhando kwani ndiye aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Tamasha la Kimataifa la Filamu Zanzibar,” alisema Tido.

Katika hatua nyingine, Tido alimtambulisha Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo kuwa ndiye wamempatia jukumu la kuwa mlezi wa tamasha la tuzo hizo litakalofanyika Februari 23, mwakani.

LihatTutupKomentar