THOMAS ULIMWENGU AANZA KWA KISHINDO SUDANI

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu usiku wa Jumamosi ameifungia klabu yake, Al Hilal Omdurman katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Al Khartoum kwenye Ligi Kuu ya Sudan.
Ulimwengu alikwenda kwa watalaamu nchini Italia kufanyishwa mazoezi maalum ya kumuweka fiti haraka arejee uwanjani, ambayo hakika yamemsaidia na sasa anajiunga na vigogo wa Sudan wanaoongoza Ligi ya kwao.
Maumivu ya goti yamekuwa yakimsakama Ulimwengu tangu alipojiunga na Eskilstuna Januari mwaka jana akitokea Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kiasi cha kushindwa kucheza.
Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya soka Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa Ligi Kuu katika klabu ya Moro United alikokuwa akicheza kwa mkopo hadi mwaka 2010 alipokwenda akademi ya AFC Eskilstuna ya Sweden, alikocheza hadi mwaka 2011 alipochukuliwa na timu ya vijana ya Mazembe.
Alicheza U-20 ya Mazembe kwa msimu moja kabla ya kupandishwa rasmi timu ya wakubwa mwaka 2012 na moja kwa moja kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza hadi anamaliza Mkataba wake Oktoba mwaka jana.
Ulimwengu alihamia Ulaya baada ya kushinda mataji makubwa akiwa na Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia.
Sasa, Ulimwengu anarejea nyumbani kujiunga na timu yake ya taifa, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa ugenini kufuzu AFCON dhidi ya Uganda Septemba 8 mjini Kampala.
Ulimwengu aliyejiunga na El HIlal Juni mwaka huu ni miongoni mwa nyota tisa wanaocheza nje walioitwa na kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa wiki ijayo Uwanja wa Mandemla mjini Kampala.


Thomas Ulimwengu (kushoto) ameifungia Al Hilal ikishinda 4-0 dhidi ya Al Khartoum kwenye Ligi Kuu ya SUDANI.
LihatTutupKomentar