HAWA YANGA MWENDO WA KINYONGA HIVI SASA WASHIKA USIKANI

Dar es Salaam. Kikosi cha Yanga, kimeifanyia kweli Coastal Union ya Ali Kiba kwa kuichapa bao 1-0, katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kupanda hadi kileleni mwa Ligi Kuu Bara.
Yanga ambayo ilipachika bao hilo dakika ya 11, likifungwa na mshambuliaji wao tegemeo, Mkongo Harieter Makambo aliyeunganisha pasi nzuri ya Ibrahim Ajibu.
Ajibu amezidi kung'ara katika kikosi hicho tangu mchezo uliopita dhidi ya Stand United, baada ya kupiga pasi za mwisho kwenye mabao yote manne waliposhinda 4-3, mechi ambayo pia ilipigwa Uwanja wa Taifa.
Itakaa kileleni ikiwa na pointi tisa sawa na JKT Tanzania wakiwa na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa hadi kesho Alhamisi.
Yanga inasubiri matokeo ya mchezo wa Mbao FC dhidi ya Simba utakaochezwa Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza pamoja na ule wa Uwanja wa Uhuru kati ya African Lyon na Singida United.
Kwani, endapo Mbao ataifunga Simba, atakuwa amefikisha pointi 10, sawa na Singida iliyo na pointi saba, itakapoifunga African Lyon.
Timu nyingine inayoweza kuongoza ni Simba kama watashinda na Mbao pamoja na Singida wakapoteza, watakuwa na pointi tisa kitakachoangaliwa ni utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa.
MATOKEO YA MECHI NYINGINE
Katika mchezo uliopigwa Musoma, Biashara United kwa mara ya pili mfululizo imeshindwa kutamba katika uwanja wake wa nyumbani wa Mandela baada ya kulazimishwa suluhu na Azam FC.
Biashara ambayo inashiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Bara, mchezo wa leo Jumatano ulikuwa wa pili katika uwanja huo wao wa nyumbani na wa tano katika Ligi.
Timu hiyo ya Biashara kabla ya mchezo huo, ilimaliza suluhu na Kagera Sugar matokeo sawa na hayo ya Azam.
Hata hivyo, suluhu hiyo kwa biashara, imetafsiriwa kama ushindi kutokana na uchanga wa timu hiyo kwenye michuano hiyo mikubwa Tanzania tofauti na ilivyo Azam.
Katika michezo mingine, Ndanda FC imeichapa Mtibwa Sugar mabao 2-1, Mbeya City imeifunga Ruvu Shooting mabao 4-2, Mwadui FC imelazimishwa sare ya 1-1, na JKT Tanzania, wakati Lipuli FC iliifundisha soka Alliance FC kwa kuifunga bao 1-0.

LihatTutupKomentar