HASSAN KESSY AVUNA KITITA KINONO ZAMBIA

BEKI wa zamani wa Yanga, Hassan Kessy, ameingia mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu ya Nkana FC ya Zambia kwa dau la Dola za Marekani 35, 000 ambazo ni takribani shilingi milioni 80 za Kitanzania.

Kessy aliondoka nchini mwanzoni mwa wiki iliyopita kwenda Zambia, ambako alifanikiwa kukamilisha dili hilo la kuitumikia timu hiyo ya Ligi Kuu Zambia.

Chanzo cha habari kutoka nchini Zambia kililiambia BINGWA jana kuwa, kimethibitisha habari hizo za kusajiliwa kwa Kessy akipewa zaidi ya dau alilokuwa akilitaka Yanga, ili kuongeza mkataba.

“Amesaini mkataba wa miaka miwili kwa dau la dola 35, 000 na tayari ameanza mazoezi na timu hiyo kwa ajili ya Ligi Kuu inayoendelea msimu huu wa 2018/19,” alisema mtoa habari huyo.

Kessy alikataa kusaini mkataba mpya na Yanga baada ya ule wa awali kumalizika kutokana na kushindwana dau na uongozi wa timu hiyo, ambapo yeye alikuwa akihitaji shilingi milioni 60 ambayo Yanga hawakuwa nayo kutokana na kuwa na ukata.

Hivyo, Kessy aliikacha Yanga na kutimkia Zambia ambako alikamilisha dili hilo na timu hiyo inayoshika nafasi ya nne ikiwa na pointi 45 kwenye msimamo wa ligi hiyo kumpa jezi namba 22.

Kessy alisajiliwa na Yanga msimu wa 2016/17 akitokea Simba kwa mkataba wa miaka miwili akiitumikia timu hiyo kwa misimu miwili kabla ya kuondoka.

LihatTutupKomentar