WANA YANGA SASA WACHEKELEA MAMBO SHWARI

BAADA ya kujiuzulu kwa Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga mchakato unafanywa klabu hiyo kuwa chini ya Abass Tarimba wakati huu wa kipindi cha mpito kabla ya uchaguzi.

Sanga alitangaza kuachia ngazi jana kwa kile alichodai kuhofia usalama wake baada ya kutishiwa amani na mashabiki na wanachama kadhaa wa Yanga.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Sanga alisema: “Naondoka Yanga nikiwa nasikitika sana… familia yangu ni bora zaidi ya Yanga, nimetishiwa amani, watu wanahamasishana kuandamana nyumbani kwangu na silaha kama wanakwenda shambani, mapanga, shoka, jembe, nimeshindwa kuvumilia.”

Mara baada ya Sanga kutangaza uamuzi wake huo, imeelezwa kuwa Bodi ya Wadhamini ya Yanga chini ya Mwenyekiti wake, George Mkuchika, ilitarajiwa kukutana jana jioni ili kumkabidhi timu Tarimba ambaye alishawahi kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo.

Mmoja wa wajumbe wa bodi hiyo, aliliambia mkomesportnews kuwa kati ya watu waliokaribu na Yanga kwa sasa, wanadhani Tarimba anafaa kuivusha klabu hiyo kwa kipindi hiki wanapojipanga kufanya uchaguzi.

“Yanga ina watu wengi tu wenye uwezo wa kuiongoza, lakini kwa sasa mtu wa haraka haraka anayeweza kuiongoza ni Tarimba… ambaye wapenzi wa Yanga wanamfahamu vizuri tu, ana uzoefu wa kutosha na anaifahamu sana Yanga,” alisema mjumbe huyo ambaye hakupenda kutajwa jina kwa madai kuwa habari hii haikutakiwa kuvuja.

Alisema baada ya Tarimba kukabidhiwa timu, atatakiwa kushirikiana na matajiri wengine wa klabu kufanya kila linalowezekana ndani ya kipindi hiki kifupi kusajili wachezaji japo wachache wenye ubora wa hali ya juu, lakini pia kumalizana na wachezaji wao wanaodai mishahara na posho nyinginezo na kuwafyeka wale wasio na msaada na timu.

“Kama unavyofahamu, dirisha la usajili linafungwa katikati ya wiki hii, hivyo tunaamini Tarimba atatusaidia kuweka mambo sawa, ikiwa ni pamoja na kumalizana na wachezaji ambao mikataba yao imemalizika.

“Nitoe wito kwa kila shabiki, mwanachama na wote wenye mapenzi mema na Yanga, kujitokeza kuisapoti timu kwa hali na mali ili tuweze kuijenga ndani ya siku hizi chache zilizobaki kabla ya kufungwa kwa usajili, lakini pia tumalizane na wachezaji wetu wanaotudai,” alisema.

BINGWA lilipomtafuta Tarimba jana kuzungumzia iwapo yupo tayari kukabidhiwa Yanga, lakini muda wote simu yake iliita bila kupokewa.

Lakini mtu wake wa karibu aliliambia mkomesportnews: “Kama alivyosema tangu awali, iwapo viongozi wababaishaji wataondoka, atafanya kila awezalo kuijenga Yanga kwani uwezo huo anao.

“Kama mnavyofahamu, tayari amemalizana na Kelvin Yondani na sasa akili yake ni kusajili wachezaji wengine wenye kiwango cha juu, akisaidiana na viongozi wengine wa kamati mbalimbali, lakini pia kuwafyeka wale wachezaji mizigo.”

Tayari imedaiwa kuwa jana usiku kuna wachezaji wapya watatu walitarajiwa kutua Jangwani kutoka Nigeria na DR Congo tayari kumalizana na mabosi wa Yanga kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo msimu ujao.

Ikumbukwe kuwa kabla ya kukaimu nafasi ya Mwenyekiti baada ya aliyekuwa akiishikilia, Yusuf Manji, kujiuzulu Mei mwaka jana, Sanga alikuwa ni Makamu Mwenyekiti.

Wakati huo huo, baada ya wachezaji kudaiwa kugoma kwa siku mbili mfululizo, kikosi cha Yanga jana kilianza mazoezi ya kujiandaa kwa mchezo wao dhidi ya Gor Mahia utakaochezwa mwishoni mwa wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Yanga inakutana na Gor Mahia katika mchezo wa nne wa hatua ya makundi wa Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupoteza mchezo wa awali kwa kufungwa mabao 4-0 wiki iliyopita na mabingwa hao wa Kenya.

Wanajangwani hao walifanya mazoezi jana asubuhi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, Dar es Salaam chini ya Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera, huku wakiwakosa nyota wao wanne.

Wachezaji walikosekana ni Andrew Vincent ‘Dante’, Benno Kakolanya, Kelvin Yondani na Hassan Kessy.

Akizungumza na mkomesportnews jana, Zahera, alisema anaendelea kufanyia marekebisho kasoro kadhaa zilizochangia kupoteza mechi iliyopita kwenye Uwanja wa Kasarani, jijini Nairobi.

Alisema hatavumilia mchezaji mvivu kwenye mazoezi yake na kama yupo, ni vizuri akajiweka pembeni mapema kwani anachohitaji ni kikosi kuwa imara na kufuata maelekezo yake.

“Mchezo na Gor Mahia najua utakuwa mgumu, lakini kinachotakiwa ni kupambana na nimewaambia wachezaji hilo, wasiwe wavivu mazoezini, tunajiandaa na mechi kubwa,” alisema Zahera.

LihatTutupKomentar