KLABU ya Lipuli imemsajili Mnigeria, Abdul Wahed Yusuph, kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaoanza Agosti mwaka huu.
Yusuph ambaye ni kiungo mshambuliaji, amepewa mkataba wa mwaka mmoja na kuchukua nafasi ya Adam Salamba aliyesajiliwa na Wekundu wa Msimbazi Simba.
Akizungumza na BINGWA, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ramadhani Mahano, alisema mpaka sasa wamesajili wachezaji wapya saba.
“Tunajua zoezi la usajili bado siku sita kabla ya kufungwa na mpaka sasa tumesajili saba na tupo kwenye mazungumzo na wachezaji wengine,” alisema.
Alisema mbali na Mnigeria huyo, wapo kwenye mazungumzo na mchezaji wao wa zamani, Joseph Owino, ili kumpa mkataba mpya.
“Tupo kwenye mazungumzo na Owino ambaye kama tukifanikiwa, tutakuwa na wachezaji wawili wa kimataifa,” alisema.
Mahano aliwataja wengine waliosajili kuwa ni beki wa Ndanda FC ya Mtwara, Job Ibrahim aliyewahi pia kuichezea Yanga SC na Issa Ally Rashid, mchezaji huru aliyesaini mkataba wa miaka miwili.
Wengine ni William Lucian ‘Gallas’ kutoka Ndanda FC, Miraji Madenge ‘Shevchenko’ na Paul John Nonga (Wote kutoka Mwadui FC ya Shinyanga), Jimmy Shoji na Rajabu Bururo ambao wote kila mmoja amesaini mkataba wa mwaka mmoja.