Mashabiki wafurika klabuni, waachwa solemba kisomi
*Kikao cha wachezaji, viongozi chaishia kwa msosi wa Kinondoni
KAIMU Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, jana alishindwa kutokea katika mkutano na wachezaji uliofanyika katika ukumbi wa makao makuu ya klabu hiyo, yaliyopo makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Japo sababu za Sanga kutokuwapo katika kikosi hicho hazikuwekwa wazi, lakini inadaiwa kuwa alihofia vurugu za mashabiki na wanachama wa klabu hiyo ambao walifurika klabuni hapo kushinikiza aachie ngazi.
Kuanzia mwanzoni hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, mashabiki na wanachama wa Yanga walikuwa wakihimizana kujitokeza kwa wingi klabuni hapo jana kuushinikiza uongozi wa Sanga na wenzake kuachia ngazi kwa kile walichosisitiza mabosi wao hao kushindwa kazi.
Kati ya mambo yaliyowafanya wapenzi hao wa Yanga kufikia uamuzi huo, ni kitendo cha timu yao kupokea kipigo cha ‘mbwa mwizi’ cha mabao 4-0 kutoka kwa Gor Mahia ya Kenya, ukiwa ni mchezo wao wa tatu wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mbali ya hilo, kitendo cha kusuasua kwa mchakato wa usajili, nacho kimechangia kupagawa kwa watu wa Yanga ukizingatia wapinzani wao wa jadi, Simba, wamefanya usajili wa kishindo kwa kunasa wachezaji wa kiwango cha juu.
Hadi sasa, Yanga imewasajili wachezaji watano tu ambao ni Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’, Mohamed Issa ‘Mo Banka’, Mohamed Jafari, Deus Kaseke, Mrisho Ngassa na Mkongomani Heritier Makambo.
Watu wa Yanga wanaamini wachezaji hao pekee hawana uwezo wa kuifanya timu yao kuwa tishio mbele ya Simba yenye wakali kama Meddie Kagere, Adam Salamba, Emmanuel Okwi, John Bocco, Asante Kwasi na wengineo wengi.
Wakiwa na shauku ya kufanikisha azma yao ya kuushinikiza uongozi kuachia ngazi, wapenzi wa Yanga waliojitokeza klabuni kwao jana, walishangaa kuona wachezaji wao wakiingia kwa ajili ya mkutano na mabosi wao.
Wakati wakisubiri kuona nini kitaendelea, baada ya saa tano walishtukia wachezaji wakitoka na kuhimizwa kuingia kwenye magari fasta bila kufahamu nini kinaendelea.
Mara mmoja wa wapambe wa viongozi wa Yanga, alisogea karibu na mashabiki hao na kuwaambia kuwa wachezaji wanapelekwa sehemu kukutana na Mwenyekiti wao aliyejiuzulu, Yusuf Manji.
Lakini baada ya muda, taarifa zilizagaa kuwa wachezaji hao walipelekwa Kinondoni kupata chakula cha mchana baada ya kushindwa kufikiwa kwa mwafaka katika kikao hicho, hapo ndipo wapenzi hao waliokuwa nje ya jengo la klabu yao walipobaini kuwa wameachwa solemba kisomi.
Juu ya kilichojiri kikaoni, mmoja wa wachezaji wa Yanga aliliambia mkomesportnews kuwa, walichotaka kufahamu kutoka kwa viongozi wao ni suala la fedha zao wanazodai na si vinginevyo.
“Tunashangaa viongozi wakaanza kutuletea siasa zao eti mwezi ujao ndio tunalipwa fedha zetu zote hivyo tuendelee na mazoezi, jambo ambalo hatukukubaliana nalo na mwisho wa siku kikao kilivunjika,” alisema mmoja wa wachezaji nyota wa Yanga.
Alisema kuwa japo wameambiwa leo wanaendelea na mazoezi Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, Dar es Salaam, lakini hadhani kama watajitokeza wengi kwani hata nauli kwao imekuwa ni shida.
Viongozi waliohudhuria kikao hicho cha jana ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hussein Nyika, Makamu wake, Mustafa Ulungo na matajiri wa klabu hiyo, Hussein Ndama, Mussa Katabaro na wengineo.
Lakini kabla ya kikao hicho, mashabiki na wanachama kadhaa wa Yanga waliojazana nje ya jengo lao, walikuwa wakipiga kelele kuutaka uongozi wa Sanga kujiuzulu, kabla ya kutulizwa na wapambe wa mabosi wao hao wakiwapa maneno matamu kuwa Mwenyekiti wao, Manji, yupo njiani kurejea kuendelea kuwasapoti.
Mkomesportnews lilifanya jitihada za kumtafuta Sanga kuzungumzia sababu za kutokuwapo katika mkutano huo na hali halisi iliyopo ndani ya klabu hiyo, lakini muda wote simu yake ilikuwa haipatikani.