JAMHURI KIHWELO AMPA SHAVU ALI KIBA

Dar es Salaam. Sahau na maneno yake ya shombo na yanayovutia mashabiki wa soka nchini, Kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo 'Julio' amekitazama kiwango cha mwimbaji wa muziki wa kizazi kipya nchini, Ali Kiba na kudai hata Yanga angecheza.
Kiba amekuwa akihusishwa kutua kwa Wagosi wa Kaya, Coastal Union waliorejea Ligi Kuu Bara, lakini Julio alisema kwa uwezo alionao hata Simba ama Yanga angeweza kutua na kukinukisha kisawasawa, ila mashabiki wengi hawajui tu.
Alisema kwa uwezo aliona KIba kuna uwezekano mkubwa wa kwenda kuwanyang'anya namba wachezaji waliopo Simba na Yanga ambao wameshindwa kufanya kazi iliyowapeleka katika klabu hizo kubwa.
"Mfano mzuri ni katika mechi ya ngao ya hisani walioiandaa Kiba na Mbwana Samatta, mwimbaji huyo aliupiga mwingi kama vile ndio kazi yake, ikumbukwe katika kikosi chake wapo walioshindwa kufunga lakini akatupia kiulaini," alisema.
"Ndio maana nimesema akisaini Simba au Yanga atacheza katika kikosi cha kwanza kwani mguuni kwake kuna madini yanayoweza kuibeba timu husika, pengine kuliko walionao ambao wanavuta mkwanja mrefu," alisema Julio beki wa zamani wa CDA, Pilsner na Simba.
Naye mwenyekiti wa Coastal Union, Steven Mguto alikiri kufanya mazungumzo na staa huyo na kudai kama atakubaliana nao wanaamini ataleta msisimko mkubwa kwa mashabiki wao kujitokeza kwa wingi kuwaangalia wanapokuwa na mechi.
"Unapotaja jina la Ali Kiba unataja supastaa mkubwa nchini, naamini akisaini sio tu ataisaidia timu lakini pia atasaidia Coastal kuongeza mapato kwa mashabiki watakaojitokeza uwanjani kumshuhudia akicheza," alisema Mguto.

LihatTutupKomentar