Licha ya kumalizana vizuri na mabosi wa Yanga juzi, unaambiwa hali pale Jangwani si nzuri kutokana na mpango wa kukipeleka kikosi kuweka kambi Morogoro kukwama.
Katika kikao walichokaa juzi viongozi wa Yanga pamoja na wachezaji wa timu hiyo kilikuwa na lengo la kujadili juu ya mgomo baridi ambao umekuwa ukifanywa na wachezaji wakidai stahiki zao.
Safari ya kuelekea Morogoro ambayo ilipasw kufanyika jana ilikwama tena na badala yake programu ya kuendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi ikaendelea japo wachezaji baadhi wakigoma kwenda kushiriki mazoezi hayo.
Nyota aliyesajiliwa kutoka Simba kuelekea msimu wa 2017/18, Ibrahim Ajibu alikuwa miongoni mwa ambao hawakufika kwenye mazoezi hayo majira ya asubuhi.
Wachezaji wengine ni beki Hassan Kessy, kipa Beno Kakolanya, Andrew Vincent pamoja na Kelvin Yondani ambaye alitegemwa kuhudhuria mazoezi hayo baada ya kukutana na Abbas Tarimba siku kadhaa zilizopita.
Haijajulikana kama safari hiyo itakuwepo tena au la kutokana na mgomo huo ambao wachezaji wamekuwa wakiuendeleza ambapo walipaswa kuondoka jana kuelekea Morogoro kwa ajili ya kambi maalum kujiwinda dhidi ya Gor Mahia FC katika mchezo wa mkondo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa jijini Dar es Salaam, Julai 29 2018.