MARCEL BONAVENTURE KAHEZA MCHEZAJI BORA WA MWEZI APRIL

MSHAMBULIAJI wa Majimaji FC ya Songea mkoani Ruvuma, Marcel Kaheza amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Aprili wa ligi luu ya Vodacom (VPL) Tanzania Bara.

Kaheza ametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda John Bocco na Emmanuel Okwi wote wa Simba ya katika uchambuzi uliofanywa na kamati ya tuzo hizo.

Kaheza aliisaidia Majimaji akifunga mabao saba (7) kwa mwezi huo, ambapo kati ya mabao hayo matatu ‘hat trick’ alifunga katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting.

Kwa mwezi huo Majimaji ilicheza michezo minne na kupata pointi saba, baada ya kushinda michezo miwili, kutoka sare mmoja na kufungwa mchezo mmoja, ikipanda kutoka nafasi ya mwisho iliyokuwepo mwezi Machi, hadi ya 14 kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo.

Kwa upande wa Bocco aliisaidia Simba mwezi huo kupata pointi 16 na kuendelea kuongoza ligi hiyo ikishinda michezo mitano na kutoka sare mmoja, huku Bocco akifunga mabao manne, wakati Okwi naye alichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio hayo ya Simba ikiwa ni pamoja na kufunga mabao matatu. Kwa mwezi huo Simba ilicheza michezo sita.

Kutokana na ushindi huo, Kaheza atazawadiwa tuzo, king’amuzi cha Azam na fedha taslimu shilingi milioni moja kutoka kwa wadhamini Vodacom.

LihatTutupKomentar