KOCHA Mkuu wa Azam, Aristica Cioaba ameondoka nchini na kuachana na klabu hiyo aliyokuwa anaifundisha.
Cioaba awali alisimamishwa kwa muda usiojulikana na kamati ya kusimamia ligi. Hivyo alikuwa anasubiri hukumu yake kutoka katika Kamati ya Nidhamu ya TFF, baada ya kumtolea maneno machafu mwamuzi kwenye mchezo dhidi ya Njombe Mji.
Kocha huyo aliyekuwa anamaliza mkataba wake na Azam mwishoni mwa msimu, ameshamalizana na mabosi wake na kuamua kurejea kwao Romania.
Aliliambia Mwanaspoti amekuwa na maisha mazuri ndani ya kikosi hicho, lakini haikuwa bahati yake kufanya vizuri.
"Nilikuwa na vijana wengi na nilifanikiwa kuwapa nafasi, walicheza soka safi kila mmoja aliona lakini sikuwa na bahati ndani ya kikosi changu," alisema.
Cioaba aliongeza kwamba ameamua pia kuondoka ili kwenda kumalizia elimu yake ya kusomea ukocha wa leseni ya kimataifa (Pro licence).