habari kuu toka Yanga leo hii

KIKOSI cha Yanga kimezidi kupata balaa baada ya kuongezeka majeruhi katika kipindi hiki wanachojiandaa na mchezo wao wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa Oktoba 14 mjini Bukoba.

Yanga inaendelea na mazoezi, lakini baadhi ya nyota wake wakiwamo Thaban Kamusoko na Obbrey Chirwa wakiwa nje wakiuguza majeraha yao.

Akizungumza na Nipashe jana, Meneja wa timu hiyo Hafidh Saleh, alisema kuwa Kamusoko na Chirwa wameungana na Donald Ngoma na Amisi Tambwe ambao nao ni majeruhi.

“Tunaendelea na mazoezi, lakini kikosi chetu kinazidi kuandamwa na majeruhi, Chirwa na Kamusoko nao wameumia na hawafanyi mazoezi,” alisema Saleh.

Alisema kuwa wachezaji hao wamepewa mapumziko mpaka Jumatatu watakapoangaliwa tena hali zao kabla ya kuruhusiwa kuanza mazoezi.

“Wamepewa mapumziko mpaka Jumatatu na baada ya hapo ndio tutajua hatima zao,” alisema Saleh.

Kama wachezaji hao watakuwa wanaendelea kujiuguza kuna uwezekano mkubwa wasiwepo kwenye safari ya Yanga kuelekea Bukoba kuumana na Kagera Sugar.

Yanga imepanga kuondoka Jumatano kuelekea Bukoba kwa ajili ya mchezo huo utakaochezwa Oktoba 14 kwenye Uwanja wa Kaitaba.
LihatTutupKomentar