MSUVA MALAWI HAWATOKI

Mshambuliaji wa Taifa Stars, Simon Msuva amewataka watanzania kujitokeza kwa wingi siku ya Jumamosi kuishangilia timu yao ya taifa.
Stars itamenyana na timu ya taifa ya Malawi maarufu kama The Flames kwenye dimba la Uhuru siku ya Oktoba 7 kwenye mchezo wa kirafiki wa FIFA.
Akizungumza na TFF TV, Msuva aliwataka mashabiki kujitokeza kuwapa sapoti ili waweze kufanya vizuri kwenye mchezo huo.
“Jumamosi tuna mechi nzuri na ngumu dhidi ya Malawi na naamini kila Mtanzania anataka kuona matokeo mazuri ambayo yametokea kwenye mechi iliyopita tulivyocheza na Botswana.

 “Mimi naomba waje kwa wingi kuishangilia timu yao, kikubwa ni kutuamini na sisi tunawapenda na watuombee kwasababu bila sapoti yao sisi hatuwezi kufanya vizuri.
“Waje kwa wingi na naamini hatutawaangusha kwa uwezo wa Mungu,” alisema Msuva anayechezea klabu ya Al Jadida ya nchini Morocco.
Stars inayonolewa na kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga ipo kambini ikijiandaa na mchezo huo ambapo inafanya mazoezi kwenye uwanja wa Boko ikiwa na nyota wake kadhaa wanaocheza soka nje ya nchi kama vile nahodha Mbwana Samatta, Simon Msuva, Abdi Banda na wengine.
Mechi iliyopita, Stars iliichabanga Bostwana kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Uhuru Septemba 2 kwa mabao yaliyofungwa na Simon Msuva akimalizia pasi za Mzamiru Yassin na Shiza Kichuya. 
LihatTutupKomentar