Usajili Yanga: kitendawili kizito katika usajili wa nyota hawa



Mnigeria Henry Tony Okoh na Mkameruni, Fernando Bongyang wako kwenye kikosi cha Yanga wakiendelea kufanya majaribio.

Na kwa kuwa klabu inakamilisha usajili wa kiungo Papi Kabamba Tshishimbi itabaki nafasi moja kwa wachezaji wa Kimataifa.

Mpaka sasa wote wameonyesha viwango vya kuridhisha kwenye siku mbili walizoonekana dimbani baada ya kumalizika kwa mazoezi ya Gym.

Dirisha la usajili litafungwa Agosti 06 kwa hivyo Yanga ina chini ya siku 10 kuamua yupi asajiliwe.

Henry Tony Okoh

Beki huyu ametoka klabu ya Akwa United inayoshiriki Ligi Kuu Nigeria.

Ni beki kisiki anayejua kukaba kwa nguvu na kutopitika kwa kirahisi akitumia miguu yote miwili, huku urefu wake ukiwa ndio silaha muhimu.

Kocha Lwandamina anataka asajiliwe beki wa kati mmoja mwenye uwezo wa kutumia mguu wa kushoto kutokana na kukosa beki mwenye uwezo huo.

Ukiangalia 'physique' ya huyu jamaa pamoja na kimo chake, kwa hakika utakubaliana na mimi kuwa Yanga haipaswi kumuachia aondoke.

Yanga inayokusudia kufanya vizuri kwenye michuano ya Kimataifa inahitaji mabeki aina ya Okoh.

Fernando Bongyang

Huyu ametokea Cameroon na amewahi kuwa nahodha wa kikosi cha timu ya Taifa ya Cameroon kwa wachezaji wa ndani kwenye michuano ya CHAN mwaka 2015.

Bongyang ni kiraka, licha ya kumudu vyema nafasi ya kiungo mkabaji, huyu jamaa pia hucheza nafasi ya beki wa kati.

Aina ya uchezaji wake inafanana kabisa na ile ya Vicent Bossou. Yuko taratibu lakini yuko makini na hufanya maamuzi sahihi kwa wakati muafaka.

Hata hivyo Okoh anaonekana kuwa vyema sana kwenye nafasi ya beki wa kati.

Mwalimu Lwandamina ana kazi ya kuamua yupi asajiliwe na ndio maana anajipa muda zaidi wa kuwaangalia mazoezini.

Lakini kama usajili wa Tshishimbi utakamilika ni dhahiri Okoh ndiye atakayekuwa mchezaji sahihi katika nafasi moja ya Kimataifa itakayobaki.

Hii ni kwa sababu Tshishimbi atamaliza shaka kwenye nafasi ya kiungo mkabaji na atasaidiana na Pius Buswita ambaye tayari ameshasajiliwa.

Bongnyang atakuwa hahitajiki. Lakini kama usajili wa Tshishimbi utakwama jambo ambalo halitarajiwi, basi wanaweza wakasajiliwa wote wawili.

Jambo jema ni kwamba Yanga huenda pia ikashusha viunge wengine wawili mahiri kumaliza kabisa utata kwenye nafasi ya kiungo.
LihatTutupKomentar