Akizungumza wakati wa sherehe ya kumuapisha waziri mpya wa Haki na Masuala ya Kikatiba Dkt Mwigulu Nchemba, bwana Magufuli alisema kwamba anasubiri ushauri kutoka kwa washauri wake kuhusu hatua atakayochukua.
''Napendekeza kwamba tuanzishe mechi za ligi yetu ya soka , lakini watu wataruhusiwa kutazama katika runinga. Nasurbiri ushauri wa wataalam ili ligi iendelee'', alisema katika hotuba ilipeperushwa moja kwa moja kutoka nyumbani kwake Chato Geita.
Tanzania iliripoti kisa chake cha kwanza cha Covid-19 tarehe 16 mwezi Machi. Tangu wakati huo, idadi hiyo imeongezeka maradufu hadi 480.
Kati ya visa hivyo wagonjwa 167 wamepona na wameruhusiwa kujiunga na familia zao nyumbani huku watu 16 wakiripotiwa kufariki.
Tarehe 16 mwezi Machi , taifa hilo lilitangaza kufungwa kwa shule kuanzia zile za chekechea hadi fomu 6 kwa siku 30.
Akizungumzia kuhusu soka, rais Magufuli amesema kwamba hakuna ushahidi kwamba wale wanaofanya mazoezi wanaweza kuathiriwa na mlipuko wa Covid-19.
'Inawezekana kwamba tutaishi na Covid-19 kama vile ambavyo tumekuwa tukiishi na virusi vya ukimwi na magonjwa mengine'', alisema.