KUFUATIA nafasi iliyopata timu ya Yanga kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, kocha mkuu wa klabu hiyo Mwinyi Zahera ameutaka uongozi kusimamisha usajili kwa wachezaji wa kimataifa kwa lengo la kuongeza nguvu katika usajili huo.
Zahera ambaye anaambatana na timu ya taifa ya nchini DRC katika michuano ya AFCON, pia atatumia nafasi hiyo kutafuta wachezaji wenye kiwango kwa ajili ya kuichezea Yanga msimu ujao.
Mpaka sasa Yanga imeshatangaza usajili wa wachezaji watano wa kimataifa na kocha huyo ameona ni vizuri kuacha zoezi hilo ili naye aangalie kwa jicho la kiufundi aina ya wachezaji watakaomfaa ili kutimiza idadi ya wachezaji 10 walioruhusiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Akizungumza baada ya kikosi cha Yanga kushika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na kukosa ubingwa Zahera alisema anafikiria kutimua wachezaji wengi kwa vile hawakuonyesha kiwango, lakini siku chache baadaye uongozi wa klabu hiyo ukamuongezea mkataba kiungo Papy Tshishimbi ili aendelee kukipiga katika klabu hiyo.
DIMBA linatambua kwamba muda mfupi tangu uongozi mpya wa Yanga chini ya Mwenyekiti wake Dkt Mshindo Msolla ukabidhiwe mikoba hiyo, umepanga usajili ambao utaimrisha timu na kurudisha imani ya Wanayanga kwa klabu yao.
Zahera amewatoa hofu Yanga akidai safari yake AFCON licha ya kuwa maalumu kwa ajili ya timu ya taifa ambayo yeye ni kocha msaidizi, pia itakuwa na manufaa kwa Yanga.
Yanga imepata nafasi ya kuungana na Simba kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku Azam FC na KMC ya Kinondoni zikipata nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho. Nafasi hiyo kwa Tanzania imekuja baada ya kuwa katika nafasi 12 bora kwenye viwango vya ubora vya CAF.
Kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu Bara zilizofanyiwa marekebisho na Kamati ya Utendaji baada ya kupatikana nafasi nne, timu za Tanzania zitakazowakilisha kwenye mashindano hayo ni Simba na Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na washindi wa Kombe la FA, Azam FC na KMC wakicheza Kombe la Shirikisho (CAF).