MIAKA 29 YA LIVERPOOL BILA UBINGWA WA EPL SOMA HAPA ILIVYOKUA MWAKA WA MWISHO KUTWAA UBINGWA

Na Godfrey Mgaya
Mambo yalivyokua wakati Liverpool ikitwaa taji la ligi miaka 29 iliyopita
Ligi kuu England (EPL) imeisha Juzi kwa Manchester City kuibuka na ubingwa. Lakini moja ya habari kubwa zaidi ni namna gani klabu ya Liverpool ilivyoupoteza ubingwa huo kwa alama moja tu.
Mara ya mwisho kwa Liverpool kushinda ubingwa wa Ligi wa England ilikuwa ni miaka 29 kamili iliyopita. Walitawazwa mabingwa wa England kwa mara ya mwisho Aprili 28,1990.
Tokea hapo klabu hiyo imekuwa ikijaribu kwa kila hali kulitwaa tena taji hilo bila mafanikio. Kuna misimu kama huu uliokwisha Liverpool walikaripia kabisa kulinyakua kombe hilo lakini bahati haikuwa kwao.

Historia inaonekana kutokuwa upande wa Liverpool katika mbio za kuwania ubingwa wa EPL.
Imekuwa ni jambo la kawaida kwa timu ambayo inaongoza EPL wakati wa msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya kuchukua ubingwa.
Katika misimu 11 iliyopita ya EPL, ubingwa ulienda kwa klabu iliyokuwa ikiongoza ligi kwenye msimu wa siku kuu hizo mara nane, na katika mara tatu pekee ambazo haikuwa hivyo yaani msimu wa 2008-09, 2013-14 na 2018-19 ni Liverpool ndiyo ilikuwa kwenye usukani.
'Dunia ya Liverpool' mwaka 1990
Mambo yamebadilika sana tokea Liverpool walipochukua ubingwa kwa mara ya mwisho. Ukitaka kujua ni namna gani miaka imekimbia huku mashabiki wa Liverpool wakendelea kusubiri furaha ya kunyakuwa kombe kubwa zaidi nyumbani kwao, inakupasa uangalie mambo yalivyokuwa kipindi hicho.
Wakati Liverpool ikitwaa ubingwa, kibao cha muziki kilichokuwa kikitikisa dunia kwa mujibu wa chati ya nyimbo 100 bora za Billboard kilikuwa kinaitwa Nothing Compares 2 U kilichoimbwa na Sinéad O'Connor kutoka Ireland. Mwezi mmoja baadae kibao maarufu cha It Must Have Been Love
kilichoimbwa na kundi la Roxette kutoka Sweden. Kibao hicho kwa sasa utakisikia pale zinapopigwa nyimbo maarufu za zamani ama 'zilipendwa'.
Kwa Afrika Mashariki muziki maarufu kwa sasa ni Bongo Flava unaozalishwa Tanzania, lakini kipindi Liverpool inachukua ubingwa wa England, Bongo Flava ilikuwa haijazaliwa.
Mwaka huo wa 1990, dunia ilikuwa na watu bilioni 5.2 wakati sasa watu wapo bilioni 5.7, hiyo ni sawa na kusema watu bilioni 2.5 hawakuwa hai mara ya mwisho Liverpool wakichukua ubingwa wa ligi.
Kikosi cha sasa cha Livepool kina wachezaji 27, Ni wachezaji watano tu kati ya hao walikuwa hai wakati timu yao ikinyakuwa ubingwa huo kwa mara ya mwisho. James Milner alikuwa na miaka minne, Adam Lallana na Simon Mignolet walikuwa na miaka miwili, Daniel Sturridge na Dejan Lovren mwaka mmoja.
Nahodha wa sasa wa klabu hiyo, Jordan Henderson alizaliwa miezi miwili baada ya ubingwa yaani Juni 1990.
Kwa upande wa siasa, Waziri Mkuu wa Uingereza kipindi hicho alikuwa ni Bi Magreth Thatcher maarufu kama 'mwananmke wa chuma' na mpaka sasa Uingereza imeshapata Mawaziri Wakuu watano zaidi.
Rais wa Kenya kipindi hicho alikuwa ni Daniel Arap Moi, ambaye alifuatiwa na Mwai Kibaki na sasa Uhuru Kenyatta ambaye kabakisha miaka mitatu uongozini.
Ali Hassan Mwinyi alikuwa katikati ya kipindi chake cha urais nchini Tanzania, baadae akapokewa kijiti na Benjamin Mkapa, kisha Jakaya Kikwete na sasa Magufuli kabakiza mwaka mmoja kumaliza muhula wake wa kwanza wa miaka mitano madarakani.
Yoweri Museveni kipindi hicho alikuwa ni miongoni mwa marais wapya Afrika akiwa madarakani kwa miaka minne tu, sasa ana miaka 33 madarakani.
Kipindi hicho bado siasa za vyama vingi zilikuwa marufuku katika nchi nyingi barani Afrika.
Jinsi Liverpool ilivyoukosa ubingwa msimu huu
Ni vigumu kuamini kuwa wakati mwaka 2018 unaisha, Liverpool walikuwa wanaongoza msimamo wa ligi wakiwaacha Manchester City kwa alama tisa.
Kilichotokea baada ya hapo ni hadithi ya Mikasa na kusikitisha kwa Liverpool.
City na Liverpool zilikutana Januari 3 huku Liverpool ikiwa inaongoza ligi kwa alama saba na kuwa na uwezekano wa kujikita kileleni kwa alama 10.
Liverpool hata hivyo walipoteza mchezo huo kwa goli 2-1 na kufanya pengo lipunguwe na kufikia alama nne.
Januari 29, City walifungwa na Newcaste goli 2-1. Liveroop walikuwa na wasaa wa kutanua pengo kwa alama 7 laiti wangeliwafunga Leicester City siku moja mbele.
Hata hivyo Liverpool ilitoka sare ya 1-1 katika mchezo huo uliopigwa Januari 30, na kufanya pengo liwe alama tano.
Februari 2, Manchester City iliwabamiza Arsenal goli 3-1, magoli yote ya City yakifungwa na Sergio Kun Aguero.
Siku mbili baadae, yaani Februari 4, Liverpool ilirejea tena dimbani dhidi ya West Ham ambapo walitoka sare ya 1-1.
Tofauti ya alama baina ya miamba hiyo ikaendelea kupungua na kufikia alama nne, na kufanya joto liendelee kupanda.
Mwezi Februari uliendelea kuwa mbaya kwa Liverpool kwani tarehe 24 walitoka sare ya bila kufungana na Mancester United.
City wao waliwafunga Chelsea 6-0 wiki moja kabla. Timu hizo zilifikisha michezo 27 na tofauti ya alama ikawa ni moja tu.
Mwezi Machi ndipo Livepool walipigwa kikumbo na City na kuachia uongozi wa ligi.
Ilikuwa Machi 3, ambapo Liverpool walishindwa kutamba mbele ya jirani zao na mahasimu wao wakuu klabu ya Everton kwa kutoka sare ya bila kufungana.
Siku moja kabla, City waliwafunga AFC Bournemouth kwa goli moja bila.
City ikaongoza ligi kwa alama moja, na toka hapo wameendelea kushikilia usikani wa ligi kwa tofauti ya alama moja mpaka wanakabidhiwa ubingwa leo.
LihatTutupKomentar