UNAMKUMBUKA yule winga matata aliyemchambua beki wa Simba, Zana Coulibaly na kutupia? anaitwa Hassan Kabunda wa KMC, unaambiwa anakaribia kutua Yanga.
Kabunda alimchambua Coulibaly na kufunga bao la kusawazisha katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ambao ulimalizika kwa Simba kushinda mabao 2-1. Katika mchezo huo, tofauti na bao hilo winga huyo mwenye kasi alionekana mwiba katika kutokana na kiwango alichokionyesha.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, tayari Yanga imeanza kufanya mazungumzo ya awali na winga huyo aliyewahi kuwaniwa na Simba.
“Muda mrefu kocha Mwinyi Zahera amekuwa akiomba mawinga wawili wa kushoto na kulia wenye uwezo mkubwa wa kupiga krosi na kasi wakiwa ndani ya uwanja.
“Katika mahitaji yake hayo Kabunda ni mmoja wa wachezaji ambao amewataja na viongozi wameridhishwa na uwezo wao wa ndani ya uwanja na kikubwa kinachokwamisha hivi sasa ni suala la fedha.
“Hivyo, kama mambo yatakwenda vizuri, basi haraka tutamalizana naye na uzuri ni kuwa ni mchezaji mzuri mwenye uwezo mkubwa,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipoulizwa Mwenyekiti wa Mpito wa Yanga, Lucas Mashauri kuzungumzia hilo alisema: “Huu siyo muda muafaka wa kuzungumzia usajili, hivi sasa akili zetu tumezielekeza kwenye ligi na Kombe la Shirikisho.” Alipoulizwa Ofisa Habari wa KMC, Anwar Binde kuzungumzia hili alisema:
“Sina uhakika wa hilo lakini kama ni hivyo huenda ikawa kweli, kwa sababu yeye mkataba wake unamalizika Desemba, mwaka huu. “Yanga hii siyo mara ya kwanza kuonyesha nia ya kumsajili, walishawahi kumuhitaji msimu uliopita sijajua sababu ya kushindwa kwenda huko,”alisema Binde.