TIMU ya Azam FC imeendeleza wimbi la ushindi baada ya kuichapa Kagera Sugar mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza jioni ya leo.
Ushindi huo umetokana na mabao ya kiungo wake, Frank Raymond Domayo dakika ya nne na mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Dombo Ngoma dakika ya 85 kwa penalti.
Kwa ushindi huo, Azam FC inafikisha pointi 62 baada ya kucheza mechi 29, ikiendelea kushika nafasi ya pili nyuma ya Yanga SC yenye pointi 67 za mechi 28.
Huo unakuwa ushindi wa sita mfululizo kwa kikosi cha Azam FC, ikiwa chini ya makocha wa muda, Idd Nassor Cheche na Meja Mstaafu, Abdul Mingange, ambao wamechukua timu hiyo mara baada ya kufukuzwa na Hans Van Der Pluijm na Msaidizi wake, Juma Mwambusi.
Walianza kwa kuichapa Rhino Rangers mabao 3-0 kwenye hatua ya 16 bora ya Kombe la FA, ikazinyuka tena African Lyon (3-1), JKT Tanzania (6-1), Singida United (4-0), Kagera Sugar (1-0) ikiwa ni ya FA na kabla ya leo kuinyuka tena Kagera (2-0) katika ligi.
Mara baada ya mchezo huo, Azam FC itaendelea kusalia tena mkoani Mwanza, ikitarajia kukipiga dhidi ya Mbao Jumapili hii, mechi itakayopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, saa 10.00 jioni.
Kikosi cha Azam FC leo; Mwadini Ally, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Lusajo Mwaikenda/Yakubu Mohammed dk 46, Agrey Moris (C), Salmin Hoza, Joseph Mahundi/Idd Kipagwile dk 87, Frank Domayo, Donald Ngoma, Obrey Chirwa/Danny Lyanga dk 72, Salum Abubakar
Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, bao pekee la mshambuliaji Iddi Suleiman 'Naldo' limeipa Mbeya City ushindi wa 1-0 dhidi ya KMC Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Kwa ushindi huo, Mbeya City inafikisha pointi 40 baada ya kucheza mechi 30 na kujiinua kutoka nafasi ya tisa hadi ya saba kwenye msimamo wa ligi ya timu 20, wakati KMC inabaki na pointi zake 41 baada ya kucheza mechi 31 katika nafasi ya tano.