Kocha Mkongo anaekinoa kikosi cha Yanga tangu msimu huu 2018/19 kuanza, Mwinyi Zahera amesema iwapo mshambuliaji wake kutoka Burundi, Hamis Tambwe atakua na kasi ya uchezaji kama mshambuliaji wa Simba Mnyarwanda Meddie Kagere atamtumia dakika 90.
“Unajua Tambwe tangu alipoumia mguu wake amebadilika, Tambwe wa sasa na wa zamani ni tofauti, nyie mmebaki na jina tu, mimi nafanya mazoezi na Tambwe nikimwambia akimbie dakika 20 au 30 atakimbia 10 au 15, siku akiwa na kasi ya mbio kama ya mchezaji wa Simba, Kagere basi atacheza kila siku, Kagere ana mbio kuliko hata viungo,” amesema Zahera
Katika mchezo wa jana dhidi ya KMC Tambwe aliingia dakika ya 74 kuchukua nafasi ya Thaban Kamusoko, hata hivyo katika mechi nyingi ambazo Zahera amekua akimtumia Tambwe amekua akitokea benchi isipokuwa mechi dhidi ya Singida aliyoanza na kuishindia timu yake magoli 2-0.