ARTURO VIDAL AFUNGUKA MAISHA YA BARCELONA



MTU anapopiga hesabu fulani hivi za maisha, mara nyingi hutarajia zitaleta matokeo mazuri, bila shaka hata Arturo Vidal alipopiga hesabu zake za kuondoka Bayern Munich na kuhamia Barcelona, alijua mambo yatakwenda vizuri.

 Hata hivyo, hesabu hizo za Vidal zinaonekana kugoma na hakuna nuru yoyote inayoonekana ikiwa imepita takriban miezi mitatu tangu atue Camp Nou na kutambulishwa kwa mbwembwe nyingi.

 Vidal, 31, kila mpenda soka anamfahamu kwa jinsi alivyo kiungo mnyumbulifu, mwenye uwezo wa hali ya juu wa kukaba pamoja na kutengeneza nafasi.

 Alifanya mambo makubwa sana akiwa na Juventus ambako ndiko alikuwa mpango mzima wa timu hiyo kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2015, na kutawala soka la Italia.

 Akiwa pale Juventus, Arturo alishirikiana vizuri na Paul Pogba pamoja na Andrea Pirlo kutengeneza safu bora ya kiungo iliyosumbua sana Italia na Ulaya kwa ujumla. Hakukuwa na sababu zozote za kiufundi ambazo zingeweza kumuweka nje ya uwanja Vidal. 

Kukosekana kwake uwanjani, lazima awe anaumwa. Alikuwa na uhakika wa namba. Hata alipokwenda Bayern Julai 2015, bado alionekana ni chaguo la kwanza linapokuja suala la kiungo.

 Msimu wake wa kwanza alicheza mechi 30 za ligi, akikosekana kwenye mechi sita tu ambazo alikuwa ni majeruhi. Aliondoka Bayern akiwa amecheza jumla ya mechi 117 za ligi. Leo hii pale Barcelona, Vidal hana nafasi. Hakuzoea maisha ya benchi, anaona ni kitu kipya. Kule kwao Chile, Vidal anachukuliwa kama Mfalme, anapokaa benchi haamini macho yake.

 Katika mchezo uliopita wa Ligi ya Mabingwa d h i di ya Tottenham kwenye Uwanja wa Wembley ambao Barcelona walishinda 4-2, Vidal aliingizwa dakika nne za mwisho, na alionyesha hasira za waziwazi. Baada ya mchezo huo, Vidal haraka aliingia kwenye mtandao wa Instagram na kuw e k a picha yake akiwa amenuna kisha kuandika maelezo haya chini yake: “Hakuna kukata tamaa. Mazuri yanakuja.

” Vidal ameanza kwenye mechi mbili tu hadi sasa akiwa na Barcelona, na inaonekana kocha  Ernesto Valverde amedhamiria kuendelea kumkalisha benchi. Akiwa benchi, Vidal amekuwa akionekana mwenye uso uliojaa simanzi. 

Hakutarajia kwamba kutoka kwake Bayern kwenda Barcelona, kungemfikisha katika hali hii aliyonayo sasa. Wakati anasajiliwa na Barcelona, aliamini anakwenda moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza, maana alitarajiwa kuwa mbadala sahihi wa Mbrazili, Paulinho ambaye alipelekwa kwa mkopo China. 

Lakini Vidal amekumbana na upinzani mkubwa wa namba kutoka kwa Sergio Busquets, Ivan Rakitic pamoja na Wabrazili watatu, Philippe Coutinho, Arthur na Rafinha. Wote hao wanawania namba katika nafasi za kiungo pale Barcelona pamoja na Vidal. 

Ukiachana na mambo yake ya uwanjani ambayo yanazidi kwenda mrama kwa Vidal, mambo ya nje ya uwanja nayo yanazidi kumvuruga Mchile huyu ambaye alifanikiwa kuibebesha Juventus ubingwa wa Serie A mara nne mfululizo kabla ya kuondoka mwaka 2015. Vidal, ambaye inaelezwa kuwa Bayern Munich inayumba kwa ajili yake baada ya kuiongoza kutwaa ubingwa wa Bundesliga mara tatu mfululizo, juzi alihukumiwa faini ya pauni 800,000 (Sh bilioni 2, milioni 386 na ushee). 


Vidal alihukumiwa na mahakama ya jijini Munich baada ya kuwa miongoni mwa genge la wahuni waliompiga na chupa ya bia jamaa fulani katika klabu moja ya usiku jijini humo Septemba. Vidal amekuwa akielezwa kwamba anapokuwa nje ya uwanja ni mtu wa kunywa pombe nyingi na kushindwa kujizuia, ndiyo maana amewahi kusababisha ajali kadhaa za gari nchini kwao Chile. Mfano, mwaka 2015, akiwa kwenye kambi ya timu ya taifa kwa ajili ya michuano ya Copa America, alipata ajali mbaya ya gari yake ya kifahari aina ya Ferrari iliyogonga gari nyingine na kusababisha akimbizwe hospitali, na alipotoka alipelekwa mahakamani na kufungiwa kuendesha gari kwa miaka miwili.   Tusubiri kuona mabadiliko, lakini mpaka sasa benchi linamvuruga sana Vidal ambaye anajiita “King”.

LihatTutupKomentar