IBRAHIM AJIBU APEWA KAZI MPYA

KAMA unadhani Kocha Mwinyi Zahera ameridhika na matokeo iliyopata timu yake mpaka sasa katika Ligi Kuu Bara, umekosea. Kwani mipango ya kocha huyo ni kama imeanza upya, baada ya kuwapa dili jipya vijana wake ili kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa mpaka mwisho wa msimu.
Kocha Zahera alisema kwa aina ya ratiba ilivyo na ugumu wa Ligi Kuu, ni lazima vijana wake kuanzia Ibrahim Ajibu, Heritier Makambo, Papy Kabamba Tshishimbi na wengine kuhakikisha wanacheza soka la kugusa na kuachia kutokana na nafasi.
Mkongo huyo alisema hataki kuona mabeki wa kati hata mara moja wanakaa au wanagusa mipira zaidi ya mara tatu nataka wakipata waokoe au kuwapatia viungo ili wasambaze mbele kwa nia ya kusaka matokeo kwa faida ya timu.
“Mabeki wa pembeni nimewambia wafanye kazi mbili kwanza kuwakaba mawinga wa timu pinzani wasipige krosi au kuingia katika eneo letu la hatari, baada ya hapo kazi nyingine ni kuhakikisha wanaanzisha mashambulizi na kwenda kupiga krosi za maana kwa washambuliaji,” alisema.
“Kiungo mkabaji napenda kumtumia Papy (Tshishimbi) lakini amekuwa akinikera kwa kukosa nidhamu nzuri ya kucheza katika eneo hilo kwani amekuwa akifanya tofauti na mimi ninavyotaka.
“Tshishimbi namueleza kazi yake ni kukaba kutokana na eneo ambalo anacheza lakini anafanya tofauti kwani anaanza kupiga chenga kama Lionel Messi jambo ambalo silitaki wala kuridhika nalo, “ alisema Zahera, aliyemsifu Feisal Salum kwa madai amekuwa katika kiwango kizuri na anafanya majukumu yake kwa ufasaha.
Alisema kwa upande wa mawinga Deus Kaseke na Mrisho Ngassa nao wamekuwa wakitimiza majukumu yao vyema kwa kupiga krosi na kutengeneza nafasi kwa washambuliaji na hata wenyewe kufunga.
Kocha huyo alisema hata kwa safu yake ya washambuliaji amewasisitiza kufanya kila njia kufunga mabao kadri wapatapo nafasi.
“Ajibu amebadilika na ananifurahisha mno kwani amekuwa akitengeneza nafasi za kufunga, anafunga mwenyewe na amekuwa mkabaji pindi mpira unapopotea, huku Makambo yeye kazi yake kwanza ni kufunga tu,” alisema.
TAMBWE, KAMUSOKO MAJINA TU
Zahera alisema anashindwa kumtumia Amissi Tambwe aliyecheza mechi ya kwanza dhidi ya Coastal Union baada ya kuumia kwa Makambo bado hafanyi vile ambavyo anataka akiwa mazoezini.
“Natambua watu wengi wanatamani kumuona anacheza Tambwe na Thabani Kamusoko kutokana na ukubwa wa majina yao lakini bado hawajafanya vile ambavyo anataka katika mazoezi.
“Majina yao ni makubwa nafahamu hilo ndio maana wanatamani kuonekana wakicheza lakini hawatacheza kama awatafanya vile ambavyo nataka katika mazoezi yangu na sitapanga wachezaji kisa majina, “ alisema Zahera ambaye atakuwa na mtihani Septemba 30 wakati atakapoikabili Simba kwenye Uwanja wa Taifa.

LihatTutupKomentar