Uongozi wa klabu ya Coastal Union ya Tanga umethibitisha kuingia mkataba na Nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Ali Saleh Kiba maarufu kama King Kiba.
Coastal wamefikia maamuzi ya kumsainisha Kiba kwa kile walichokieleza kuwa ana kipaji cha mpira na wanaamini ataisaidia klabu hiyo.
Klabu hiyo imesema tayari jina la Kiba limeshawekwa kwenye mfumo wa mpya wa usajili unaotumika hivi sasa (TFF FIFA CONNECT) ambapo dirisha la usajili Limefungwa leo majira ya saa 6 kamili usiku.
Taarifa za awali kutoka uongozi wa Coastal zilizema kuwa Kiba alikwenda mwenyewe kuomba nafasi ya kuichezea klabu hiyo kutokana na mapenzi yake ya kucheza mpira wa miguu.
Baada ya kuomba nafasi hiyo, uongozi wa Coastal Union ulianza mazungumzo ya kumalizana na Kiba na sasa atakuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo msimu ujao.
Baada ya kumalizana na nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini Ali Kiba kwa kuingia mkataba wa kuichezea Coastal Union, uongozi wa klabu hiyo umetuma salaam kwa wapinzani wake.
Kupitia Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ndani ya klabu hiyo, Steven Mguto, amesema sasa wapo na moto balaa na wakiahidi kuibuka na ushindi dhidi ya timu zote watakazokutana nazo.
Mguto anaamini kikosi cha Coastal union kitafanya makubwa na kuwashangaza wengi kwa kusema wamefanya usajili maridadi na wapo tayari kwa msimu mpya.
Ikumbukwe Coastal union iliteremka daraja msimu wa 2015/16 pamoja na klabu ya African Sports zote kutoka Tanga lakini sasa wametamba kuwa wanarejea na kishindo kikubwa.