YONDANI KUCHUKULIWA HATUA ZA KINIDHAMU

Nahodha wa Yanga, Kelvin Yondani anakabiliwa na adhabu ya kufungiwa michezo isiyopungua mitatu na faini isiyopungua Sh500,000 hadi Sh3milioni kwa kitendo chake cha kumtemea mate beki wa Simba, Asante Kwasi.

Yondani alifanya kitendo hicho, lakini mwamuzi hakuona hata hivyo picha za marudio zilionyesha tukio hilo wakati wa mechi ya watani wa jadi ililiyochezwa jana Jumapili na Yanga kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Simba.

Pamoja na kunusurika kupata kadi nyekundu kwa kitendo hicho bado Yondani anaweza kukumbwa na adhabu kali kutoka TFF na Bodi ya Ligi kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu.

Kanuni ya Kanuni 37 ya Udhibiti kwa wachezaji kipengele (7) inasema Mchezaji atakayefanya jambo lolote kati ya yafuatayo atafungiwa michezo isiyopungua mitatu (3) na faini isiyopungua sh. 500,000 (laki tano):
(c) Kumshambulia mwamuzi, kiongozi, mtazamaji au mtu yoyote kwa namna yoyote ile, iwe kwa matusi au kwa vitendo.
(d) Kufanya kitendo chochote cha aibu, kama vile kukojoa kiwanjani, kukataa kupeana mkono na mgeni rasmi, waamuzi na wachezaji wa timu pinzani, kutoa au kuonyesha ishara inayoashiria matusi.
(f) Kufanya kitendo chochote kitakachobainika kuwa ni kinyume cha maadili ya mchezo wa mpira wa miguu.

Pia, Yondani anaweza kushtakiwa kwa kanuni hiyo 37, kipengele cha namba (23) kinasema Mchezaji yeyote atakayepatikana na hatia ya kufanya makosa makubwa ya kimaadili au kinidhamu, au ya kibaguzi au ya kidhalilishaji au yatakayotafsiriwa kuwa ni ukiukaji mkubwa wa taratibu za mchezo na ubinadamu atatozwa faini kati ya sh. 1,000,000 (milioni moja) mpaka sh. 3,000,000 (milioni tatu) au/na kusimamishwa kushiriki michezo mitatu mpaka kumi ya klabu yake yoyote atakayoitumikia katika Ligi Kuu na mashindano mengine rasmi ya TFF au kufungiwa kipindi cha kati ya mwaka mmoja na miwili.

Kitendo cha nahodha huyo wa Yanga, Yondani kumtemea mate mwenzake ni uvunjifu wa kanuni 36 Uchezaji wa Kiungwana (fair play).
Kucheza kiungwana kunakujengea heshima wakati kudanganya kunaleta aibu. Kumbuka kuwa mpira wa miguu ni mchezo na mchezo wowote hauwezi kuwa na maana kama hautochezwa kiungwana kwa kuzingatia kanuni na taratibu ili mshindi halali aweze kupatikana.

Mchezo wa kiungwana unamaanisha kuheshimu wapinzani. Bila ya wapinzani kutakuwa hakuna mchezo. Kila mmoja ana haki sawa, ikiwemo haki ya kuheshimiwa. Wachezaji wa timu moja ni wenza. Tengeneza timu ambayo kila mmoja kwenye timu atakuwa na haki sawa. Waamuzi wapo kuhakikisha nidhamu na mchezo wa kiungwana unadumishwa. Siku zote kubali maamuzi yao bila ya ulalamishi, na wasaidie

waweze kuwafanya washiriki wote waufurahie zaidi mchezo. Viongozi pia ni sehemu ya mchezo na wanatakiwa wapewe heshima wanayostahili. Watazamaji wanaufanya mchezo uwe na msisimko. Wanahitaji kuuona mchezo ukichezwa kiungwana kwa kuzingatia kanuni, lakini pia wanatakiwa kuwa waungwana na kujiheshimu.
LihatTutupKomentar