UCHAMBUZI MECHI YA YANGA LEO

Na Godfrey Mgaya
MABINGWA
wa kandanda Tanzania bara, Yanga wanapaswa kucheza kwa nidhamu kubwa ya kujilinda Jumatano hii mjini Awassa, Ethiopia ili kufuzu kwa mara ya pili hatua ya makundi ya Caf Confederations Cup ndani ya miaka mitatu. Kuhusu soka la nyumbani, bila shaka Yanga ndio ‘watawala’ na kitendo cha kufuzu tena hatua ya makundi ya Caf msimu huu kutakuwa kunawatambulisha upya katika soka la vilabu barani Afrika.
Yanga wanaikabili Wolaitta Dicha katika mchezo wa marejeano wakiwa mbele kwa mabao 2-0, ushindi ambao waliupata Dar es Salaam takribani siku kumi zilizopita. Matokeo yoyote ya sare yatawapeleka katika hatua ya makundi kwa mara nyingine baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza April, 2016 walipoiondoa Esperanca kutoka Angola kwa jumla ya mabao 2-1 ( 2-0 nyumbani, 1-0 ugenini)

Mfumo wa 3-5-2utawabeba Yanga
Kocha huyu anakaimu nafasi iliyoachwa na George Lwandamina wiki iliyopita na mchezo wake wa kwanza unaweza kumfanya apewe kibarua cha kudumu mwishoni mwa msimu. Siwezi kusema lolote kwa sasa kuhusu kocha huyo ambaye alikuwa sehemu ya benchi la ufundi la Mzambia mwenzake, Lwandamina.
Kwa aina ya kikosi alichonacho huko Ethiopia, Mwandila anapaswa kuichezesha Yanga katika mfumo wa 3-5-2.Kuwapanga walinzi watatu wa kati, Kelvin Yondan, Abndallah Shaibu na Vicent Andrew kutaifanya safu ya mashambulizi ya Dicha ambayo inaonekana kuwa na wachezaji wawili wasumbufu ishindwe kufurukuta vile inavyotakiwa.
Makapu, Tshishimbi, Raphael, Abdul na Gadiel
Said Juma Makapu, Mcongoman, Papy Tshishimbi na kijana Raphael Daud wakiunga na Juma Abdul katika wing-back ya kuume, Gadiel Michael katika upande wa kushoto kutaifanya Yanga kuwa imara katikati ya uwanja. Katika mchezo wa Dar es Salaam, Dicha walionekana kukosa stamina ya kutosha, huku uwezo wa mchezaji mmoja mmoja ukiwa si wa kiwango cha timu inayoweza kusumbua katika michuano ya kimataifa.
Yanga wanatakiwa kujilinda vizuri, kucheza kwa nidhamu na kuepuka kucheza faulo karibu na eneo lao la hatari kwa maana mipira iliyokufa wakati mwingine imekuwa ikizibeba timu nyingi zenye wapigaji mahiri na bado hatuwezi kusema moja kwa moja kuwa Dicha si wazuri katika upigaji wa mipira iliyokufa kwa maana hawakupata kabisa katika mchezo wa kwanza.
Kujilinda kwa kumiliki mpira kwa muda mwingi ndicho wanachopaswa kufanya Yanga na kitendo cha kuwaweka wachezaji hao nane niliowataja kunaweza kuwapa wakati mgumu Dicha kwa maana kimbinu timu hiyo ya Ethiopia ilionesha awali bado hawako katika ubora wa kuisumbua Yanga. Muhimu ni kucheza kwa kufuata maelekezo ya benchi la ufundi na namna ya wachezaji kutumia maarifa binafsi.
Wanapoteza sana mpira wakiwa maeneo ya kati na wanapokuwa wakishambulia huwa wanaacha nafasi nyingi za wazi katika ngome yao, na hii inaweza kuwapa Yanga nafasi ya kuwaadhabu hasa kwa kutegemea mipira mirefu ya kupenyeza kutoka kwa Juma na Gadiel, na wakati mwingine kutoka kwa Tshisimbi na Raphael.

Chirwa na Buswita katika mashambulizi

Kumpanga Obrey Chirwa kama mshambulizi wa kwanza na Pius Buswita karibu yake naona itawafaa zaidi Yanga kwa maana walinzi wa kati wa timu hiyo walionekana kukatika mno wakati walipokutana na kinda Yusuph Mhilu katika uwanja wa Taifa. Chirwa ni mtulivu na wakati anapoingia ndani ya eneo la hatari hujenga kujiamini zaidi.
Kama, Raphael angekuwa mtulivu katika mchezo wa kwanza angeweza kufunga magoli zaidi ya lile moja alilofunga, hivyo pacha ya Chirwa na Buswita inaweza kuwapa Yanga walau goli moja muhimu ugenini jambo ambalo litawalazimu wenyeji wao kushinda ushindi wa zaidi ya magoli manne jambo ambalo sitaraji litokee hata kidogo kwa maana Dicha si timu kali, muhimu kucheza kwa kuwaheshimu tu.
Hii ni nafasi ya wazi kwa Yanga kujitangaza tena katika soka la Afrika na kitendo cha mabingwa hao mara tatu mfululizo wa ligi kuu bara kufuzu kwa hatua ya makundi kutaisaidia nchi huko mbele kuongezewa timu katika michuano ya Caf.
Kwa sasa Tanzania bara inapeleka Caf wawakilishi wawili tu, hii inatokana na klabu zetu kushindwa kuwika kila mwaka na ili kupata nyongeza ya wawakilishi wengine wawili-mmoja katika Champions league na mwingine Canfederation ni lazima klabu zetu zifuzu makundi walau kwa misimu mitano mfululizo.

LihatTutupKomentar