MAISHA YA DILUNGA NDANI YA MANUNGU

Na GODFREY MGAYA
Kiungo wa Mtibwa Sugar Hassan Dilunga amesemaanafurahia maisha ya Manungu ambako ndio makao makuu ya klabu yake ya sasa na kusema anaamini maisha yake bado yataendelea kuwa mazuri ndani ya klabu hiyo.
Dilunga amejiunga na Mtibwa akitokea JKT Ruvu ‘sasa JKT Tanzania’ baada ya timu hiyo kushuka daraja, aliwahi pia kucheza Yanga lakini hakudumu kwa muda mrefu kwa sababu ya kukosa nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwana.
Tangu ajiunge na Mtibwa kiwango chake kimeimarika kwa kiasi kikubwa huku akipata nafasi ya kucheza ndani ya kikosi cha kwanza cha kocha Zubery Katwila, licha ya timu yake kupoza mbele ya Simba kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro Dilunga alicheza kwa kiwango cha juu katika mchezo huo.
Maisha ya Manungu
Toka nimejiunga na Mtibwa naona maisha yangu yapo vizuri, yanaendelea kuwa vizuri na yatazidi kuwa vizuri. Maisha na wachezaji wenzangu kwa ujumla yapo vizuri tunashirikiana na kufurahi pamoja kila kitu kipo sawa nimefurahi sana kwa kupata ushirikiano mkubwa tunasaidiana kila jema na lisilo jema.
Mchezaji yeyote unapokwenda kwenye timu mpya lazima utapata changamoto kwa sababu utakutana na wachezaji ambao wapo siku zote utaanza kugombea nafasi pamoja na mambo mengine.
Dilunga amejiunga na Mtibwa na kufanikiwa kupata nafasi moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza, nini siri ya mafanikio?
Ni kujituma zaidi na kusikiliza mwalimu anataka nini na kufanya kwa ufasaha kitu ambacho mwalimu anakihitaji ndio kumeleta mafanikio hadi nimepata namba.
Support kwa mama ‘kija’
Najisikia faraja kwa sababu kama uliona mchezo wa Lipuli dhidi ya Mtibwa nilifunga goli kipindi ambacho mkewangu alikuwa ni mjamzito halafu mimi niko mbele nyuma ipo familia yangu, ukizungumza familia yangu unazungumzia mke wangu na mtoto wangu ndiyo maana nilitoa ishara ya kumsapoti mkewangu kwa kitu ambacho amekuwa nacho.
Amepata kidume
Pia hivi karibuni nilifanikiwa kufunga kwenye mchezo dhidi ya Singida United nikatoa ishara ya kumsapoti mkewangu na mwanangu kwa sababu tayari alikuwa ameshajifungua mtoto wa kiume.
Penati ya kwanza vs Azam
Hivi karibuni Mtibwa iliifunga Azam kwa penati katika mchezo wa robo fainali ya Azam Sports Federation Cup baada ya timu hizo kutoka sare ndani ya dakika 90, Hassan Dilunga alipiga penati ya kwanza kwa upande wa Mtibwa Sugar.
Nilijisikia furaha kubwa kupewa penati ya kwanza kwa sababu naamini benchi la ufundi lilikuwa na imani na mimi kwa kitu ambacho nilitakiwa kufanya kwa sababu tulishafanya mazoezi ya penati kwa hiyo nilijisikia furaha na nilijiamini zaidi. Kupewa penati ya kwanza kulinifanya nifikirie kuhusu watu wanne wa nyuma yangukwa hiyo mimi nilitakiwa kuonesha mwelekeo na ndiyo maana nilipiga penati nzuri.
Kabla ya mchezo wa Azam, mida kama ya saa 7 mchana nilipokea taarifa kutoka kwenye familia yangu kwamba mkewangu amejifungua salama mtoto wa kiume ambaye alipewa jina la Nizar. Kilikuwa kitu kigeni kwa siku hiyo na ilikuwa kama surprise na nilikuwa na nahamu kubwa ya kumpa zawadi mkewangu pamoja na mwanangu ambaye ndiyo alikuwa amezaliwa.
Niliwapa taarifa wachezaji wenzangu nikawaambia naomba mnipe zawadi siku ya leo, nashukuru walijituma wakanipa zawadi nilifurahi sana.
Mchezo utakuwa mgumu kwa sababu kila hatua ambayo mnafika kila mtu anajiandaa kwa sababu unakaribia kufika sehemu fulani kwa upande wetu tunauangalia mchezo kwa jicho la pili tutajiandaa zaidi na zaidi kwa sababu Stand ni timu nzuri na sisi ni timu nzuri lakini hatuwezi tukasema kwamba tutashinda tutajipanga ili tufanye vizuri katika huo mchezo.
Mtibwa bingwa FA Cup
Dilunga anasema anaiona nafasi ya Mtibwa ni kubwa kushinda taji la Azam Sports Federation Cup 2018 mbele ya timu nyingine tatu ambazo zimefuzu kucheza nusu fainali ya kombe hilo.
Asilimia 100 naiona Mtibwa inaenda kuwa bingwa wa FA Cupkwa sababu toka tumeanza ligi tulikuwa na malengo yetu kwenye ligi kuu na kwenye FA, kama wachezaji watakuwa wanakumbuka na wanatarajia malengo tuliyoyaweka, tutafanikiwa kuchukua ubingwa.

LihatTutupKomentar