CANNAVARO AHAIDI MAKUBWA KESHO

Nahodha na beki kisiki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, amesema kuwa mechi yao na watani wao, Simba wala haina umuhimu kwao kutokana na wao kuwaza fedha ambazo wataingiza baada ya kutinga katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga wanaoshika nafasi ya pili kwenye ligi wakiwa na pointi 47 watakutana na Simba katika pambano la ligi ambalo linatarajiwa kupigwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar Aprili 29, mwaka huu ambapo pambano hilo ndilo litatoa taswira juu ya timu ipi itatwaa ubingwa kwa msimu huu.
Pia kikosi hicho cha Yanga kilisafiri usiku wa kuamkia jana Jumapili kuelekea Ethiopia kwa ajili ya kwenda kuvaana na wenyeji wao Wolatya Dicha katika mchezo wa mkondo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika ambao utapigwa nchini humo keshokutwa Jumatano.
Cannavaro ambaye ameiongoza Yanga kutwaa ubingwa misimu mi­tatu mfululizo, ameliambia Championi Jumatatu, kuwa mchezo wao dhidi ya Simba wala hauwaumizi kichwa kutokana na kutokuwa muhimu sana kwa kuzingatia mwenendo wa ligi ulivyo bali wana­chokiangalia kwa sasa ni mechi ya marudiano na Dicha ambapo kama wakifuzu hatua ya makundi watakunja kiasi kikubwa cha fedha.
“Hiyo mechi na Simba kwa sasa siyo muhimu sana kwa sababu kwanza iko mbali tofauti na mchezo wetu huu wa marudiano dhidi ya Dicha ambao kama tukifanikiwa kusonga mbele kuna donge kubwa la fedha ambazo tutazipata tofauti na tukikomaa na ligi.
“Kwangu mimi naona ni bora tukiweka akili zetu juu ya mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Wolayta Dicha na siyo kitu kingine, tukimalizana nao ndipo tutaanza kufikiria juu ya mechi zijazo za ligi,” alisema Cannavaro.
Iwapo Yanga itafanikiwa kusonga mbele kwenye hatua ya makundi ya kombe hilo la shirikisho Afrika itakuwa imejiingizia fedha katika nafasi yoyote ile ambayo watashika. Ikiwa ya nne katika kundi itapata milioni 336, wa tatu milioni 536, wa pili milioni 536 au wakiwa mabingwa wa kombe hilo watajikusanyia bilioni 1.8.

LihatTutupKomentar