KUZIONA AZAM NA SIMBA BUKU TANO TUU JMOS HII

MCHEZO wa Ngao ya Jamii kuashiria kupenuliwa kwa pazi la Ligi Kuu ya Tanzania Bara utafanyika Jumamosi wiki hii (Agosti 17, 2019) kuanzia Saa 1:00 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Mchezo huo utawakutanisha mabingwa wa Ligi Kuu, Simba SC dhidi ya washindi wa KOmbe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC).
Taarifa ya TFF leo imesema kwamba viingilio katika mchezo huo vitakuwa vya madaraja mawili tu, Sh 5,000 kwa majukwaa ya mzunguko na Sh. 10,000 kwa maeneo ya VIP B na C.


Simba SC ndio mabingwa wa Ngao ya Jamii msimu uliopita baada ya kuichapa Mtibwa Sugar 2-1 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Agosti 18, mwaka jana.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Elly Sasii aliyesaidiwa na Hellen Mduma wote wa Dar es Salaam, na Ferdinand Chacha wa Mwanza, mabao ya Simba SC yalifungwa na mshambuliaji Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere dakika ya 29 kiungo Hassan Dilunga dakika ya 45, wakati la Mtibwa lilifungwa na mshambuiaji chipukizi, Kelvin Sabato Kongwe au Kiduku dakika ya 33.
Hiyo ilikuwa mara ya nne kwa Simba SC kutwaa Ngao ya Jamii, baada ya 2011 wakiifunga Yanga 2-0, 2012 wakiifunga Azam FC 3-2 na mwaka 2017 wakiwafunga tena mahasimu wao wa jadi, Yanga kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0.
Azam FC yenyewe imetwaa Ngao ya Jamii mara moja tu, 2016 walipoifunga Yanga kwa penalti 4-1 baada ya sare ya 2-2 kati ya mara tano ilizowania.
2012 walifungwa 3-2 na Simba SC, 2013 walifungwa 1-0 na Yanga SC, 2014 walifungwa 3-0 na Yanga SC na 2015 walifungwa na Yanga SC kwa penalti 8-7 baada ya sare ya 0-0.

LihatTutupKomentar