Mabao ya Ally Ramadhan mnamo dakika ya 51 kipindi cha pili na Japhet Makalai katika dakika ya 79 yameiwezesha Kagera Sugar kusalia kunako Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Kagera imefanikiwa kupata ushindi huo wa mabao 2-0 ikiwa ni baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika matokeo yakiwa ni 0-0 dhidi ya pamba kutoka jijini Mwanza.
Matokeo hayo yanairejesha rasmi Kagera Sugar kunako ligi na itakuwa moja ya timu za msimu mpya ujao wa 2019/20.
Katika mechi ya mkondo wa Mwanza jijini Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Kagera na Pamba zilitoka suluhu ya kutofungana.
Ikumbukwe walima miwa hao wa Kaitaba mkoani Kagera waliingia hatua ya Play Off baada ya kumaliza ligi ya msimu huu wakiwa na alama 44 katika nafasi ya 18 ya msimamo wa ligi.
Mbali na Kagera kusalia, Mwadui FC kutoka Kishapu, Shinyanga nayo imesalia katika ligi kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Geita Gold Mine.
Ushindi huo umepatikana kupitia mabao ya Salim Aiyee aliyeingia kambani mara mbili kunako dakika za 33 na 90+3 huku bao pekee la Geita likifungwa na Baraka Jerome katika dakika ya 50.
Kupoteza kwa Geita Gold kunawafanya waungane na Pamba kuendelea kusalia Ligi Daraja la Kwanza kwa ajili ya kupambania nafasi nyingine tena ya kusaka tiketi ya kupanda Ligi Kuu Bara kwa msimu unaokuja