Aliyoyazungumza Mwekezaji Mkuu wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji Mo kuelekea mechi ya kesho na TP Mazembe.
"Tumejipanga vizuri sana, ari ya wachezaji wetu ni kubwa na Mungu akitujalia basi kesho tutafanya maajabu. Mimi kilichonileta hapa ni kuwaomba mashabiki wa Simba, Watanzania wajitokeze kwa wingi uwanjani"- Mo Dewji.
"Kujitokeza kwa mashabiki kuna faida kuu mbili, moja unawaongezea nguvu wachezaji wetu na wao wanaona kuwa Watanzania wapo nyuma yao, lakini pili inawaogopesha wapinzani wetu"- Mo Dewji.
"Niwashukuru mashabiki wa Simba, niwapongeze ukiangalia takwimu za mechi za Ligi ya Mabingwa hakuna timu ambayo imejaza uwanja wake kama Simba Sports Club, Simba inaongoza kwa kujaza uwanja kwenye mechi zake"- Mo Dewji.
"Nawaomba sana mashabiki ikitokea bahati mbaya ya hapa na pale, tuendelee kushabikia sio tu mpaka tukipata goli, naomba sana tubadilike kwenye hilo, tushangilie Simba tangu mwanzo hadi mwisho"- Mo Dewji.
"Hapa hatushiriki tu, tunajiamini kwamba tunaweza na tunataka kwenda mbali zaidi ya hapa"- Mo Dewji.
"Shabaha yetu sio tu kufanikiwa mwaka mmoja, tunataka kushinda kombe kila mwaka ili tushiriki Ligi ya Mabingwa kila mwaka, tunataka kushinda kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika, mimi naamini uwezo tunao, tumtangulize Mungu"- Mo Dewji