UKISIKIA tu mshambuliaji Jacques Tuyisenge ameshatambulishwa Simba SC, basi jua kuwa kila timu itakayokutana na Simba itakuwa inakula si chini ya mabao 3-0.
Tusiyenge alipoulizwa na mkomespornews jana jijini hapa alizuga kwamba hajafanya mazungumzo rasmi na Simba lakini yuko tayari kuwapokea muda wowote. Mkomesportnews linajua kwamba Simba wameshamcheki kwenye simu lakini anafanya siri mpaka mipango yote ikae sawa.
“Niko tayari kuzungumza na timu yoyote kwa sababu mkataba wangu na Gor Mahia unamalizika Desemba, mwaka huu na hawajaniambia kama wanataka tuongeze,” alisema staa huyo jijini hapa.
“Ishu ya Simba haijaja rasmi mezani kwangu nimeisikia tu, mimi napendelea sana nchi zinazoongea Kifaransa, Kiswahili na Kinyarwanda.
“Dili nilizonazo sasa ni kutoka AS Vita na timu nyingine za Cyprus lakini akili yangu iko kwa Gor Mahia zaidi sasa kwa vile nina mkataba nao,” alisisitiza mchezaji huyo ambaye ni swahiba mkubwa wa Meddie Kagere wa Simba.
Simba chini ya mwekezaji mkubwa, Mohammed Dewji ‘Mo’ imepanga kufanya usajili mkubwa wa kimataifa kwenye dirisha kubwa lengo ni kuhakikisha wanafikia mafanikio ya juu zaidi kimataifa msimu ujao. Hivyo Simba imepanga kufanya usajili kwa umakini mkubwa na kuzingatia matakwa ya benchi la ufundi chini ya Mbelgiji, Patrick Aussems.
Championi ambalo ndilo gazeti la kwanza kuandika ishu ya Simba kuwa mbioni kumsaini Tuyisenge anayechezea Gor Mahia ili akacheze na pacha wake Meddie Kagere, limethibitishiwa na wakala wa mchezaji huyo, Patrick Gakumba kuwa sasa kila kitu kinakwenda sawa.
Gakumba ameweka wazi kwamba Tuyisenge akishatua tu Simba basi kila timu watakayokuwa wakikutana nayo itakuwa inakula mabao zaidi ya matatu kwa bila hivyo ukipiga hesabu kwa mechi 38 ambazo Simba itacheza kwenye ligi pekee jumla itafunga mabao 114.
Aliongeza anaamini Kagere na Tuyisenge kwamba wakicheza pamoja watafanya maangamizi makubwa kwa timu pinzani ndiyo maana anapenda kuona wateja wake hao wakicheza pamoja ili kuisaidia Simba itishe zaidi Afrika. Gakumba ambaye muda mwingi anapenda kutabasamu, aliongeza kuwa hata Tuyisenge anapenda kuungana na Kagere ili kuiendeleza ile pacha yao na kutupia mabao mengi.
Alisema anapenda kuona Simba inafanikiwa kimataifa na kuwa moja kati ya klabu kubwa Afrika ndiyo maana anataka kuwapa Tuyisenge ili akaongeze nguvu itakayowafanya watishe msimu ujao kwenye ligi ya ndani na michuano ya kimataifa.
“Kwanza nikwambie mimi ndiye wakala wa Kagere na Tuyisenge. Nataka hawa wacheze pamoja tena kama ilivyokuwa Gor Mahia ili Simba itishe zaidi Afrika.
“Wakiwa pamoja kila timu watakayocheza nayo watakuwa wanakula si chini ya mabao 3-0, na uzuri yeye mwenyewe (Tuyisenge) anaipenda sana Simba.
“Mchakato wa kuhakikisha hili linafanyika unaendelea vizuri hivyo naomba watu wasubiri usajili,” alisema Gakumba