YANGA HII NI BALAAA YAENDELEA KUWAKIMBIA WATANI WAKE

Na
Godfrey Mgaya
Ndio! Mabingwa wa kihistoria wa Tanzania Yanga wameilaza Tanzania Prisons mabao 3-1 katika dimba lao la Sokoine katika mchezo ambao nusura uvurugwe na maamuzi mabovu

Tanzania Prisons ilipewa penati ya utata mwishoni mwa kipindi cha kwanza na Jumanne Elifadhili akaifungia timu hiyo bao la kuongoza.

Penati hiyo ilipingwa vikali na wachezaji wa Yanga kupelekea Ajib, Chikupe na Ngasa kuonyeshwa kadi za njano baada ya kumzonga mwamuzi.

Kabla ya tukio hilo Ibrahim Ajib na Heritier Makambo walifanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari la Prisons lakini mwamuzi hakuchukua hatua yoyote.

Presha ya mchezo ilipelekea Mrisho Ngasa kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kichwa Laurance Mpalile ambaye naye pia alitolewa nje baada ya kufanya tukio hilo hilo

Kipindi cha pili Yanga iliingia na kasi kubwa ikisaka bao la kusawazisha.

Mabadiliko ya kocha Mwinyi Zahera kwa kumtoa Juma Abdul na kumuingiza Amisi Tambwe yaliinufanisha zaidi Yanga kwani Tambwe aliyecheza kwa dakika 18 ndiye nyota wa mchezo huo.

Kwenye dakika ya 76 Yanga ilipata penati baada ya mlinzi wa Prisons kuunawa mpira uliokuwa umepigwa na Heritier Makambo ndani ya eneo la hatari

Makambo alipokea pasi kutoka kwa Tambwe. Ajib aliisawazishia Yanga kupitia penati hiyo.

Tambwe akaifungia Yanga bao la pili kwenye dakika ya 85 akiunganisha krosi ya Matheo Anthony kisha akafunga la tatu kwenye dakika za majeruhi baada ya kutumia vyema makosa ya mlinzi wa Prisons.

Wachezaji wa Yanga, kocha Mwinyi Zahera na benchi lake la ufundi wanastahili pongezi kwa kazi kubwa waliyoifanya mkoani Mbeya leo.

Yanga imeibuka na ushindi uliopatikana katika mazingira magumu sana, kuanzia hali ya uwanja baada ya mvua kubwa kunyesha na matukio ya ndani ya uwanja.

Ushindi huo umeikita Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 38, alama tano mbele ya Azam Fc inayoshuka dimbani kesho.

Aidha Yanga imeiacha Simba kwa alama 11!

LihatTutupKomentar