Licha ya Nkana FC Jumamosi iliyopita kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba, lakini mashabiki wa timu hiyo wameonekana kukata tamaa ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hali hiyo imekuja muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa kwanza wa hatua ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa kwenye Uwanja wa Nkana uliopo hapa Kitwe, Zambia.
Muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo huo, mashabiki wa Nkana ambao ni raia wa Zambia, waliishiwa nguvu na kuonyesha sura za kukata tamaa wakiamini kwamba katika mechi ya marudiano hawataweza kuwaondoa Simba.
Ili Nkana ifuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo, inatakiwa kulinda ushindi wake huo katika mechi ya marudiano, wikiendi ijayo jijini Dar es Salaam.
Lakini kutokana na kiwango kilichoonyeshwa na Simba ikiwemo kupata bao moja ugenini, ndiyo inawafanya Wazambia hao kuamini kwamba licha ya kushinda, lakini hawawezi kuvuka.