KOCHA SIMBA AIPIGIA HESABU TP MAZEMBE

KIKOSI cha Simba, kinaendelea na tizi kwa ajili ya mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya African Lyon, ikiwa siku chache tangu ilipobanwa mbavu na watani wao, Yanga, lakini akili ya Kocha Patrick Aussems ikiwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha Aussems anafahamu vijana wake wanaweza kukutana ama na TP Mazembe, Al Ahly ama klabu nyingine zilizotamba kwenye nchini zao, hivyo ameamua kuanza mapema kujipanga ili kuhakikisha wanafanya vyema katika michuano hiyo ya CAF.
Simba inaendelea kujifua kwenye Uwanja wa Boko Veterani, kwa ajili ya mchezo dhidi ya Lyon ambao kuna wasiwasi wa kuwakosa nyota wake wanne waliopo timu ya taifa, lakini Aussems anafichua akili zake zipo kwenye michuano ya CAF itakayoanza Novemba 29.
Nyota atakaowakosa Mbelgiji kwenye mechi yake ya keshokutwa ni Jonas Mkude, Aishi Manula, Shomary Kapombe na John Bocco ingawa nyota hao wanaruhusiwa kwenda kufanya majukumu yao klabu hapo, lakini Aussems awapigii sana hesabu.
Kocha huyo alisema kwa kiuwa ana kikosi kipana haoni tatizo kuwakosa nyota hao, lakini akisisitiza kuwa mkazo wake kwa sasa ni mechi za kimataifa zilizopo mbele yake akidai atatumia mfumo walioucheza dhidi ya Yanga kuwabana Mazembe au Al Ahly ya Misri.
"Nafahamu tutakutana na timu kubwa Afrika kama Al Ahly, Esperance, TP Mazembe na nyingine, ila kwa mpira tuliouonyesha dhidi ya Yanga nadhani ndio nitakaotumia dhidi ya klabu hizo kubwa, kwani timu ilicheza vizuri, licha ya kushindwa kupata matokeo."
"Malengo yetu ni kufika hatua ya makundi kisha tukifanikiwa hapo tutakuwa na malengo mengine ya kwenda mbele zaidi ndio maana tunafanya maandalizi ya kutosha ili timu kubadilika na kucheza vizuri huku ikipata ushindi katika kila mechi," alisema Aussems.
Mbelgiji huyo aliyeiwezesha Simba kubeba Ngao ya Jamii, huku ikikusanya alama 11 katika mechi zake sita, alisema ana muda wa mwezi mmoja na ushei kabla ya kuanza kazi michuano ya CAF ndio maana anaanza mapema kujipanga ili kufanya makubwa.
NIYONZIMA, JUUKO FRESHI
Kiungo Haruna Niyonzima na beki Juuko Murshid ambao hawakuwa katika kikosi cha Simba kwa muda mrefu, kabla ya kurudishwa hivi karibuni, zile wiki mbili walizopewa na Kocha Aussems zimeisha na sasa wakati wowote wataanza kuliamsha.
Kwa sasa wachezaji hao wamerejeshwa kwenye programu za kawaida za mazoezi na nyota wengine, baada ya kupikwa vilivyo na Kocha Msaidizi, Masoud Djuma.
Mbelgiji aliwapa programu ya siku 14 chini ya Masoud ambayo imemalizika hivyo kazi imebaki kwao kupambana ili kupata namba kwenye kikosi cha Mbelgiji huyo.
"Kazi itakuwa kwao kupambana na kuhakikisha wanaingia kikosi cha wachezaji 18 ambao nawatumia katika mechi husika lakini kwangu nimewaangalia na nimelidhika nao kuwa wana uwezo wa kushindana na kuisaidia timu kufikia malengo yake.
"Kwangu nimemaliza jukumu langu la kuwaangalia na watarudi katika programu za wachezaji wote ambao nawatumia kila mechi lakini jukumu litabaki kwao kutokana nafasi ambazo wanacheza kuwa wachezaji ambao wanafanya vizuri.
"Uwepo wao nadhani ushindani utaongezeka kwa kila mmoja ili kutamani kupata nafasi ya kucheza na hata yule ambayo anacheza hatakubali kutoka atashindana na kufanya vizuri ili kuendelea kucheza," alisema Aussems
MANARA NAYE
Katika hatua nyingine Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara ameliomba Shirikisho la Soka (TFF), kuangalia kwa jicho la mbali zaidi timu ya Taifa aliyodai ni muhimu ipate matokeo mazuri ili ifuzu kucheza Afcon ambayo Tanzania ilishiriki mara ya mwisho mwaka 1980.
"Hofu yangu ni kuona kwamba ligi inaweza kuwa na ratiba ngumu hapo baadaye kwani kama Simba itaenda kucheza mashindano ya Kimataifa na malengo yetu ni kufika hatua ya makundi kwa maana hiyo mechi zetu zitaghailishwa na kusogezwa mbele.
"Kingine Simba, Yanga na Azam mwakani Januari zitashiriki Kombe la Mapinduzi kwa wiki mbili, hivyo mechi za ligi zitasogezwa, naomba mamlaka husika kuangalia ratiba hii la sivyo ligi inaweza isimalizike Mei kama ilivyopangwa," alisema Manara.

LihatTutupKomentar