FEISAL TOTO AZIDI KUIMARISHA SAFU ZA VIUNGO


Dar es Salaam. Kombinesheni ya viungo wa Yanga, Papy Tshishimbi na Feisal Salum 'Fei Toto' inafanya vizuri licha ya kutokuwa pamoja kwa kipindi kirefu.
Uwepo wa Kocha Mwinyi Zahera aliyechukuwa mikoba ya Mzambia George Lwandamina aliyerudi kuifundisha timu yake ya zamani ya Zesco, alibadili namna uchezaji wa viungo wake.
Zahera alimchezesha Tshishimbi kama kiungo mchezeshaji licha ya kwamba awali alikuwa akicheza kama mkabaji, huku Feisal ambaye alikuwa akicheza kama mchezeshaji akicheza kama kiungo mkabaji.
Katika nafasi hiyo ya kiungo, amemwongezea pia, Ibrahim Ajib kwa ajili ya kuongeza nguvu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fei ambaye amekuwa nyota katika kikosi cha Yanga kwa sasa, amesema ana uwezo wa kucheza sehemu yoyote kikubwa ni kutimiza majukumu.
“Mimi ni kama jembe la shamba, popote ambapo nitawekwa nitacheza, kikubwa ni kufuata maelekezo ya kocha na kufanya kazi yake vizuri kama ambavyo anahitaji kazi ifanyike, kikubwa kwamba kwa upande wangu nazidi kuimarika,” alisema.

LihatTutupKomentar