ZAHERA HACHEKI NA MTU MOROGORO



Yanga jana Jumatano walianza kambi yao mkoani Morogoro chini ya kocha wao mkuu, Mwinyi Zahera kwa kujiandaa na mechi dhidi ya Simba Jumapili hii ambapo kocha huyo alianza kuwanoa washambuliaji wake kuwa makini kwenye kumalizia nafasi ambazo wanazitengeneza.

Zahera raia wa DR Congo alianza kuwanoa washambuliaji wake wakiongozwa na Heritier Makambo kwenye mazoezi hayo yaliyofanyika katika Chuo cha Biblia mkoani Morogoro.

Mmoja wa wachezaji wa Yanga ameliambia Spoti Xtra kuwa kocha huyo nje ya kuwanoa washambuliaji hao pia aliwapa somo walinzi wake juu ya kuokoa mipira ya krosi kwa kutumia vichwa.

“Tulianza mazoezi kwa kuzunguka kwa kukimbia mara sita baada ya hapo tukaanza kufanya mazoezi ya mbinu ambapo kocha aliwapa mbinu washambuliaji pamoja na mabeki.

“Kwa washambuliaji walikuwa wakifundishwa jinsi ya kutumia nafasi za kufunga, kwa kutumia krosi halafu wanaunganisha kwa vichwa na miguu pamoja na kupiga mashuti.

 “Na mabeki wenyewe walikuwa wakifundishwa jinsi ya kuokoa mpira ya krosi kwa kutumia vichwa, hicho ndicho ambapo tulikifanya leo (jana) kwenye mazoezi yetu, hata hivyo tulihenyeshwa sana,” alisema mchezaji huyo.

 Hata hivyo kumekuwa kukionekana kuwa na ulinzi mkali sana kwenye mazoezi na kambi ya Yanga huku wachezaji na kocha wakipigwa marufuku kuzungumza na waandishi au mtu yeyote anayefika kambini hapo.

LihatTutupKomentar