HAMISI TAMBWE AWATAMANI SIMBA

Dar es Salaam. Mabao mawili aliyofunga Amiss Tambwe dhidi ya Singida United, yamegeuka silaha katika mchezo ujao na watani wao wa jadi Simba.
Yanga ilitoka uwanjani kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-0 iliyopata juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, umempa morali ya kufanya vyema katika mchezo huo.
Miamba hiyo ya soka, inateremka uwanjani Jumapili wiki hii kumenyana katika mchezo unaotarajiwa kuwa msisimko mkali kutokana na rekodi ya timu hizo msimu huu.
Tambwe alisema endapo Kocha Mwinyi Zahera atampa nafasi ya kucheza atafanya maajabu katika mchezo huo.
Alisema amerejea kwa kishindo baada ya kupona jeraha la goti lililomsumbua muda mrefu, lakini amepona na matarajio yake ni kurejesha makali ya kufunga mabao.
"Nahitaji kurejea kwenye kiwango changu na rekodi ya ufungaji bora, nafarijika nimeanza vizuri msimu, katika mchezo wa kwanza niliopangwa nimefunga mabao mawili, hiyo ni faraja kubwa kwangu.
"Tunaelekea kwenye mchezo mgumu dhidi ya Simba ingawa sipendi kuizungumzia timu hiyo, lakini kama nikipata nafasi ya kucheza siku hiyo sitafanya kosa," alisema Tambwe.
Akizungumzia mabao aliyoyafunga dhidi ya Singida United, Tambwe alisema matarajio yake ni kuifunga timu yake hiyo ya zamani.
"Sio jambo la ajabu kufunga kwa sababu ni kazi yangu uwanjani, labda mashabiki wanaweza kushangaa kwa vile hawajaniona muda mrefu nikicheza kutokana na majeraha," alisema Tambwe.
Tambwe aliyewahi kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu misimu miwili tofauti alipokuwa Simba na baadaye Yanga, alisema amekuwa akiumiza kichwa kutafakari namna ya kufunga mabao.
"Hakuna mshambuliaji asiyependa tuzo ya mfungaji bora, binafsi natamani kuichukua tena msimu huu, lakini pia timu kutwaa ubingwa, japo ni mapema lakini siku zote mwanzo mzuri unakuwa na mwisho mzuri naamini ndoto yangu itatimia mwishoni mwa msimu," alisema nyota huyo raia wa Burundi.
LihatTutupKomentar