HIVI karibuni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilitoa agizo la kuzitaka klabu za Simba na Yanga kufanya uchaguzi ndani ya siku 75.
Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba, walitakiwa kufanya uchaguzi mkuu kwa kuwa muda wa viongozi wanaokaimu nafasi hizo umeshapita.
Lakini Yanga kwa upande wao walitakiwa kufanya uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi zilizo wazi kwenye uongozi wao kutokana na wengi wao kujiuzulu nafasi zao. Mpaka sasa idadi ya viongozi wa Yanga waliojizulu nafasi zao imefikia watano, ukijumlisha na Katibu Mkuu, Charles Boniface Mkwassa aliyebwaga manyanga hivi karibuni kwa madai ya matatizo ya kiafya.
Lakini kwa kuwa nafasi ya katibu mkuu ni ya kuajiriwa, Yanga watalazimika kufanya uchaguzi wa kuziba nafasi ya mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji.
Viongozi waliojiozulu nafasi hizo ni bilionea Yusuf Manji aliyekuwa Mwenyekiti, Clement Sanga, Makamu Mwenyekiti na Salum Mkemi na Hashim Abdallah waliokuwa kwenye Kamati ya Utendaji.
Kwa sasa akili za mashabiki wa Yanga zimejikita sana kwenye kujua ni nani atakayechukua nafasi ya mwenyekiti wa klabu hiyo kwa miaka minne ijayo.
Majina mbalimbali yanatajwa kuwemo kwenye mchuano huo, akiwemo mwenyekiti wao wa zamani, Yusuf Manji ambaye kama ataibuka na kukohoa tu, basi ni wazi hakuna wa kumtetemesha kwenye nafasi hiyo.
Lakini ukimya wa Manji mpaka sasa kama atarudi kwenye nafasi yake au la, umewaibua vigogo wengine wanne wanaotajwa kuwa na uwezo wa kuitoa Yanga katika dimbwi la ukata linalowatesa hivi sasa.
Vigogo hao ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, Tarimba Abbas Tarimba, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, Abdalah Bin Kleib, huku mwingine anayetajwa pia ni mlezi wa klabu ya Singida United na Mbunge wa Iramba Mashariki, Dk. Mwigulu Nchemba ambaye ni mwanachama damu wa Yanga.
Kutokana na mchuano huo kuonekana kuwa mkali kwa wagombea wote kulingana na sifa, gazeti lako linaloongoza kwa uchambuzi makini wa habari za michezo na burudani, MKOMESPORTNEWS , lilizama chimbo na kuibuka na kigezo kikubwa ambacho Wanayanga wanatakiwa kukizingatia kabla hawajakwenda kwenye sanduku la kupiga kura.
Kwa hali ilivyo sasa na kama Manji hatarejea kwenye nafasi yake, basi wanachama wa Yanga wanatakiwa kutafuta mwenyekiti mwenye uwezo wa kutafuta kiasi cha Sh bilioni sita katika kipindi cha miaka minne atakayopata ridhaa kuiongoza klabu hiyo.
Ndio, Yanga inahitaji mwenyekiti atakayetafuta fungu hilo mbali na pesa za wadhamini wanazopata kila msimu kutoka kwa SportPesa, Azam TV, mapato ya mlangoni na mdhamini wa ligi ambaye bado hajatangazwa mpaka sasa.
Kwanini Sh bilioni 6?
Unaikumbuka Yanga iliyotikisa nchi? Yanga ile iliyokuwa na uwezo wa kumfunga mtani wao, Simba, nje ndani. Yanga iliyoweza kusajili mchezaji mmoja kwa Sh milioni 200? Unaikumbuka Yanga iliyoweza kuweka kambi ya kibabe Uturuki?
Sahau kuhusu kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo, hapa naizungumzia Yanga iliyoweza kuvitetemesha vigogo vya soka Afrika kwenye michuano ya kimataifa?
Nyuma ya mafanikio yote hayo waliyopata Yanga katika misimu ya hivi karibuni, kuna jeuri ya pesa ya aliyekuwa mwenyekiti wao, Manji.
Hivi karibuni baada ya kujiuzulu, aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, alifichua namna Manji alivyokuwa anatenga bajeti ya Sh bilioni 1.5 kila mwaka kwa ajili ya kuiendesha klabu hiyo.
“Mzigo ulikuwa mkubwa sana. Ukiangalia Manji alikuwa na bajeti kubwa sana aliyoitenga kwenye kuiendesha klabu, hivyo kuondoka kwake ilikuwa ni pigo sana kwetu tuliobaki,” alisema Sanga.
Kwa hesabu hizo, ni wazi kuwa kwa miaka minne ambayo Manji alikuwa anaiongoza Yanga kama katiba ya klabu hiyo inavyoagiza, bilionea huyu alikuwa na bajeti ya Sh bilioni sita.
Inadaiwa hizi ni fedha ambazo Manji alikuwa anazitoa katika vyanzo vyake ndiyo maana wakati fulani iliwapa kiburi Yanga kususia fedha za baadhi ya wadhamini lakini bado waliendelea kufanya vizuri.
Kuelekea kwenye uchaguzi huo ambao unatakiwa kufanyika ndani ya siku 75 kama ambavyo TFF imewaagiza, wanachama wa Yanga wanatakiwa kumbana mwenyekiti ajaye lazima awatengee kiasi hicho cha pesa ili kurudisha heshima ya timu hiyo ya kuitwa wa kimataifa kutokana na kupata fursa ya kucheza michuano ya kimataifa, huku wakionyesha soka la kuvutia.