SANTOS FC YAWATOZA MTIBWA SUGER MILIONI 34

UONGOZI wa Mtibwa Sugar umesema klabu ya Santos ya nchini Afrika Kusini, imetaka kulipwa Dola 15,000 za Kimarekani (shilingi milioni 34 za Kitanzania) kwa awamu kama fidia yao kwa maandalizi waliyofanya kujiandaa kuvaana nao.

Mwaka 2003 Mtibwa ilifungiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), kushiriki michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa miaka mitatu, kutokana na kushindwa kucheza  mchezo wa marudiano dhidi ya Santos kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao.

Mtibwa hivi sasa inajiandaa kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kubeba taji la Kombe la FA kwa kuifunga Singida United mabao 3-2, katika mchezo wa fainali uliochezwa Juni 2 mwaka huu, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Akizungumza na mkomesportnews juzi, Mkurugenzi wa klabu hiyo, Jamal Bayser, alisema pamoja na kuwa wameshailipa faini hiyo, lakini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limewataka kulipa tena kwa kuwa wao hawana uthibitisho wa malipo hayo.

Alisema wamezungumza na viongozi wa klabu ya Santos na wamewataka kulipa fedha hiyo mapema, hivyo wao hawana tatizo watapambana ili walipe na kujihakikishia ushiriki wao katika michuano ya kimataifa.

“TFF wametutaka tulipe deni hilo na tumekubali, tumeshazungumza na viongozi wa klabu ya Santos na wanahitaji kulipwa Dola 15, 000 za Kimarekani ambazo tumeomba tuwalipe kwa awamu tatu,” alisema Bayser.

Hata hivyo, aliongeza kuwa wanatarajia kuanza kulipa kuanzia mwezi huu na kumaliza Desemba mwaka huu

LihatTutupKomentar