MZEE AKILIMALI AWASHANGAA YANGA

Katibu wa Baraza la Wazee Yanga, mzee Ibrahim Akilimali, ameibuka na kumlalamikia aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga, ikiwa ni baada ya uongozi kutangaza kuomba michango ili klabu isimame vizuri.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya kaimu Katibu Mkuu, Omary Kaaya juzi kutangaza kuwa Yanga itaanzisha namba maalum ili wapenzi, wanachama, mashabiki na wadau wa klabu hiyo waanze kuichangia kutokana na kupitia kipindi cha mpito.

Kitendo hicho kimemfanya Akilimali kuanza kumshutumu Sanga kuwa ndiye alikuwa sababu ya yote hayo kutokea akielezea kitendo chake cha kuivunja kamati maalum ambayo iliundwa kuisaidia Yanga wakati mpito kupitia mkutano mkuu.

Kwa mujibu wa Radio EFM kupitia kipindi cha Sports HQ, Akilimali amehoji akisema anashangaa kwanini wanahabari wanashindwa kumuuliza Sanga vizuri juu ya kinachotokea Yanga hivi sasa kutokana na hali kuwa ngumu mpaka klabu imefikia hatua ya kuanza kuomba fedha ili ijikimu na hali ngumu kiuchumi.

Mzee huyo amefunguka na kueleza Sanga hakupaswa kuivunja ile kamati na hapo ndipo anapoamini kuwa mwanzo wa kuongeza chachu ya Yanga kufikia hapa ilipo mpaka sasa.

"Kwanini msimuulize Sanga ambaye alivunja kamati ya mpito, yeye ndiye alisababisha yote haya kutokea mbaka klabu inafikia katika hali hii" alisema.

LihatTutupKomentar