IBRAHIM AJIBU NAE KUWAFATA YANGA MORO

STRAIKA wa Yanga, Ibrahim Ajib, anatarajiwa kuungana na wenzake leo kwenye kambi ya timu hiyo iliyopo mkoani Morogoro.

Yanga waliingia kambini wiki iliyopita kujiandaa na michuano ya Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 22, mwaka huu.

Kikosi chote cha Yanga kipo kambini isipokuwa mchezaji wake huyo aliyesajili msimu uliopita akitokea Simba, ambaye alishindwa kuungana na wenzake kutokana na matatizo ya kifamilia.

Akizungumza na Mkomesportnews jana, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, alisema Ajib ataungana na wenzake leo kwenye kambi hiyo kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa kifariki dhidi ya Mawenzi Market katika Uwanja wa Jamhuri, mjini humo.

Alisema, amepewa taarifa na uongozi kuwa Ajib na Mohamed Issa ‘Mo Banka’, wote watajiunga leo na kuendelea na mazoezi pamoja na wenzao kambini hapo.

“Nimeambiwa Ajib atakuja kesho Jumatatu (leo), tayari Tshishimbi amejiunga kambini lakini tunamsubiri Ajib na Mo Banka kwa ajili ya kuendelea na programu ya mazoezi,” alisema Zahera.

Yanga inatarajiwa kucheza na Mawenzi Jumapili ikiwa ni mechi ya heshima kwa ajili ya kumuaga aliyekuwa nahodha wao wa muda mrefu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyestaafu kucheza soka na kupewa jukumu la kuwa Meneja wa timu hiyo.

Ijumaa iliyopita, Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten, alisema Ajib, Ramadhan Kabwili pamoja na Papy Tshishimbi, wangeungana na wenzao kambini huko tangu Jumamosi ambako tayari wenzake walikwenda isipokuwa yeye tu.

Katika mechi hiyo maalumu ya Yanga, kabla kutakuwa na burudani ya muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali nchini kama, Mr Blue, Afande Sele, Lulu Diva, Juma Nature na Billnas, huku Yanga Queens ambayo itaongozwa na Wema Sepetu ikicheza mechi dhidi ya Morogoro Kombaini

LihatTutupKomentar