YANGA YAZIDIWA KETE USAJIRI

IKIWA katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa kiungo wa JKU ya Zanzibar, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Yanga imezidiwa ujanja na Singida United ambayo imefanikiwa kumnasa nyota huyo.
Awali, Yanga ilikuwa kwenye mazungumzo ya mwisho kwa ajili ya kumsajili kiungo huyo ambaye alitakiwa kusajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Yanga ilivutiwa na kiungo huyo katika Kombe la Mapinduzi na michuano ya Kombe la Chalenji iliyofanyika nchini Kenya.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi kutoka Singida United, tayari timu hiyo imefikia makubaliano mazuri na kiungo huyo na kusaini mkataba wa miaka miwili kwa siri.

Mtoa taarifa amesema, Singida United walimfuata kwa siri kiungo huko Unguja, Zanzibar kwa ajili ya kumalizana naye.
“Fei Toto tayari amepewa mkataba wa miaka miwili na kikubwa tumefikia hatua hiyo baada ya kuvutiwa na kiwango kikubwa alichokionyesha kwenye michuano ya Kombe la Chalenji.

“Amesajiliwa kwa mujibu wa mapendekezo ya benchi la ufundi la Singida baada ya kuuona uwezo wake, kwani kama unavyojua Mudathiri (Yahaya) anarudi Azam (FC)

“Tulisikia Yanga wanamtaka Fei Toto kwa ajili ya kumsajili lakini tulipofuatilia tukasikia wameshindwana naye na ndiyo sisi tukamfuata na kumsajili kwa kumpa fedha na mshahara mnono,” alisema mtoa taarifa.

Alipotafutwa Meneja Mkuu wa Singida United, Ibrahim Mohamed kuzungumzia hilo alisema; “Hilo suala la kumsajili Fei Toto halijanifikia mezani na zaidi nilikuwa nasikia tetesi za kiungo huyo kusajiliwa na Yanga, ni vizuri tukasubiri kidogo.”
Fei Toto alipotafutwa alisema: “Kuna timu nimesaini lakini siwezi kuitaja kwa sasa.”

LihatTutupKomentar