Msuva awaaga mashabiki wa klabu ya Yanga



Mfungaji bora wa msimu uliopita Simon Msuva, amewaaga mashabiki na wanachama wa Yanga, baada ya mipango ya kujiunga na timu ya Difaa Hassani El Jadida ya Morocco kukamilika.

Msuva amesema anashuru sapoti kubwa na malezi bora kutoka kwa mashabiki hao hivyo wakati umefika kwa yeye kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine.

“Nawashukuru sana kwa sapoti yao tangu nimetua Yanga nikiwa kijana mdogo hadi leo nimepata mafanikio makubwa kwa sapoti yao naomba wasinichukie kwani haya ni maisha nakwenda kujaribu huko ikishindikana nitarudi Yanga,”amesema Msuva.

Kiungo huyo mshambuliaji ambaye kwasasa yupo kwenye kambi ya timu ya taifa inayojiandaa kucheza mechi ya marudiano dhidi ya Rwanda, amesema akiwa Morocco, atamisi mambo mengi ikiwemo ushindani wa Simba na Yanga.

Amesema pamoja kuwa anaondoka lakini anakiamini kikosi kilichopo kitafanya kazi vizuri na kuendelea kulinda heshima ya Yanga ambayo inafahamika Tanzania na Afrika kutokana na ubora iliyokuwa nao kwenye soka la ndani.

Amesema siku zote Yanga itabaki mawazoni mwake kwani ndiyo timu iliyompa mafanikio aliyokuwa nayo hivi sasa na kwakiasi kikubwa ndiyo imechangia yeye kuonekana na El Jadida na kuvutiwa naye.

Difaa El Jadidi imemaliza katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi msimu uliopita ikiwa na pointi 59 nyuma ya WCA Casablanca waliomaliza katika nafasi ya kwanza wakiwa na pointi 66.

Ligi kuu ya Morocco inajumuisha timu 16 kama ilivyo kwa ligi kuu Tanzania bara (VPL).
LihatTutupKomentar