TIMU ya Azam FC, iliyo chini ya Mholanzi Hans Pluijm imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba katika mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi uliochezwa leo Uwanja wa Gombani, Zanzibar na kutetea ubingwa wao.
Safu ya ushambuliaji ya Azam FC iliyokuwa ikiongozwa na Obrey Chirwa, ilionekana kuwa na uchu wa mabao tangu kuanza kwa mchezo huo.
Dakika ya 43, kiungo wa timu hiyo, Mudathiri Yahya, alifunga bao la kwanza akimalizia pasi mpenyezo ya Ennock Atta Agyei.
Iliwalazimu Simba kusubiri mpaka dakika ya 63 kusawazisha bao hilo kupitia kwa beki wake, Yusuf Mlipili aliyefunga kwa kichwa akimalizia kona iliyopigwa kiufundi na Shiza Kichuya.
Dakika ya 73, Obrey Chirwa, alikamilisha karamu ya mabao kwa Azam FC kufuatia kuunganisha kwa kichwa krosi safi ya Nicholas Wadada.
Kwa matokeo hayo, yameifanya Azam FC kufanikiwa kutetea ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya tatu mfululizo. Walianza kuchukua mwaka 2017, 2018 na sasa 2019, hivyo linakuwa kombe lao jumlajumla.
Baada ya kuibuka mabingwa, Azam imekabidhiwa kombe, medali za dhahabu na fedha kiasi cha shilingi milioni 15.